Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Alhamisi, Novemba 19, 2020

Alhamisi, Novemba 19, 2020,
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa

Ufu 5:1-10;
Zab 149:1-6, 9;
Lk 19:41-44

JE, TUNAPATA UTUKUFU KATIKA YERUSALEMU YA ZAMANI AU KATIKA YERUSALEMU MPYA?

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo katika adhimisho la Misa Takatifu. Leo wimbo wetu wa katikati ni wa shukrani ukimshukuru Mungu kwa kutufanya kuwa wanaukoo wakifalme na kikuhani tuweze kumtumikia yeye. Ndio sababu za kufurahi katika wimbo wetu wa katikati.

Katika somo letu la kwanza, tunagundua kwamba aliyetutendea haya ni Yesu mwenyewe kwa sababu yeye hakuogopa au kuona aibu au kufa moyo. Alikubali kuchinjwa na kwa damu yake akaweza kutununua. Na kama asingalifanya hivi, hakika angalikosekana wa kukifungua kitabu au chuo kinachozungumziwa leo katika somo letu la kwanza. Kitabu hiki kilikuwa cha muhimu kwani ndicho kilichobeba ujumbe kuhusu mpango wa Mungu juu ya ulimwengu. Na kweli kama Yesu asingalikuwa mtii hakika asingalitokea wa kuweza kukitwaa hicho kitabu na kikifungua.

Sisi ndugu zangu tunahitajika tukakifungue kitabu, Mungu anapenda kututumia kufungua kitabu na hivyo basi lazima tuwe na utii na tuepukane na majivuno. Halafu ni lazima tuwe watu wa sadaka zaidi, tusikatishwe tamaa kirahisi tuvumilie. Hivi vilimsaidia Yesu. Sisi tuache uvivu; ukitukanwa au kujibiwa vibaya tu usilalamike kana kwamba ni mtu kakuua. Bado songa mbele.

Katika injili, Yesu anaeleza hasara ziwapatazo wale walio na kiburi. Yerusalemu ilikuwa hivyo. Ilitawaliwa na watu waliojiona kuwa wanaweza kila kitu wakifikiri kwamba umaarufu wa mji utawaokoa; sio hivyo.
Yesu anawaambia kwamba mtashangaa mtakapoona kwamba mji wenu wote unaangushwa.

Somo hili linatuhusu sisi tulio na kiburi. Wengi tunafikiri kwamba akili zetu zitatuokoa, au kitendo cha kuwa kiongozi kanisani, labda mwenyekiti wa halimashauri ya walei au uongozi mwingine, au mwenyekiti wa chama cha kitume ndio inakuwa tayari nimeshaokoka, au kwa kitendo cha kushinda kanisani nimeshaokoka. Hapana. Wokovu hupatikana katika bidii na unyenyekevu. Lazima tuwe watu wa kufanya bidii, tujione kuwa hatustahahili. Hapa ndio tutashinda.

Tukifikiri ati tutashinda kwa hela au akili au kwasababu nina kazi nzuri serikalini au kwa nguvu zetu kamwe hatutaweza kusonga popote. Tukiwa na mali au uwezo wa kiakili alafu tukakosa unyoofu tunapoteza ladha kabisa. Tupambwe na unyenyekevu Yesu atatusifu.Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni