Jumatatu, Novemba 16, 2020
Jumatatu, Novemba 16, 2020,
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa
Ufu. 1:1 – 4; 2:1 – 5
Zab. 1:1 – 4, 6 (K) Ufu. 2:7
Lk. 18:35-43
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Naomba tafakari yetu iongozwe na maneno ya wimbo wa katikati kwamba yule ashindaye atampatia nafasi ya kula katika mti wa uzima.
Kiitikio hiki kinatualika kubakia imara hadi mwisho kwani vishawishi ni vingi na anayetunzwa ni yule tu anayebakia kuwa imara hadi mwisho. Wengi huwa tunaanza vyema lakini shida ni kudumu hadi mwisho.
Zaburi hii inatumika kutusaidia katika kulitafakari somo la kwanza hasa kwa ule ujumbe wa kanisa la Efeso. Kanisa hili lilianza vyema kiimani tangu Paulo alipohubiri huko Injili. Walikataa falsafa za kipagani na kuwapinga baadhi ya wale wakristo ambao walirubuniwa na mafundisho ya uongo na kuingiza falsafa katika mafundisho ya Kristo na mwishowe wakaishia kuupoteza ukristo kabisa.
Kanisa hili lilikuwa hodari. Lakini kidogokidogo lilianza kulegea na ufunuo wa Yesu leo unaliambia likazane zaidi liongeze bidii. Ndio ujumbe ambao Yesu anataka kutuambia kila mmoja wetu siku ya leo. Yabidi nasi kuwa watu wa bidii zaidi, mara nyingi ile siku ya kufunga ndoa au kupata upadre au nadhiri au komunio au kipaimara huwa tunakuwa motomoto sana. Lakini tunaanza kupungua taratibu. Sasa ni lazima tuzidishe bidii kila wakati; huu ndio ukristo wenyewe.
Mara nyingi tunaanguka kwa sababu ya uzembe na kupunguza bidii. Sisi tuzidishe bidii yetu zaidi. Hii ndio itakayotuokoa. Kama nipo kazini nizidishe upendo na kuongea na wenzagu vizuri zaidi. Kama ni daktari niongeze bidii na kuacha uzembe wa kuhudumia. Nisikubali kupoteza uhai wa mtu kwa uzembe wangu.
Katika somo la injili, tunakutana na kipofu mmoja aliye na bidii kumwamini na kumfuata Yesu. Yeye anapokatazwa na wenzake asije kwa Yesu, moja kwa moja anaongeza bidii, anazishinda kelele za wale wanaomzuia na mwishowe anamfikia Yesu na kupata uponyaji. Sisi tuzidishe bidii ya kumtumikia Yesu. Tusitishwe na maneno ya wenzetu pembeni watakaokasirika kwa kitendo cha wewe kuacha ulevi au kuacha urafiki mbaya nao. Njia hii ndio itakayokufanya umfikie Yesu na kupata toka kwake uponyaji na kuokolewa.
Wengi tumeshindwa kubadilika kwa sababu tunatishwa sana na kelele za wenzetu walioko karibu yetu ati wanasema nini. Wakisema vibaya tu juu yetu tunaacha kile kizuri tunachofanya na kwenda kuwafuata. Hapana. Tusiishi namna hii. Tubadilike. Tuwe watu wapya wakumsikiliza Mungu anataka nini, tusiogopeshwe na maneno ya watu.
Maoni
Ingia utoe maoni