Jumatano, Novemba 18, 2020
Jumanne, Novemba 17, 2020,
Juma la 33 la Mwaka wa Kanisa
Ufu 3:1-6, 14-22;
Zab 14:2-5,
Lk 19:1-10
FURAHA YA UPENDO WA YESU
Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo kanisa linazidi kutukumbusha juu ya ujio wa nyakati za mwisho na hivyo linatualika kumrudia Mungu na kuwa na bidii zaidi.
Wimbo wetu wa katikati unatueleza kwamba yule atakayeonesha bidii hii atapatiwa nafasi ya kuushiriki utukufu mkuu utokao kwa Mwenyezi. Akina Musa, Elia na Abrahamu ni miongoni mwa watu waliojitahidi na hivyo basi waliwezeshwa kukwea mlima wa Bwana na kupewa utukufu na m
Mwenyezi Mungu. Nasi tunahimizwa kuongeza bidii tuweze kuukuta utukufu huu.
Somo letu la kwanza linaendeleza mada hii kwa undani zaidi. Katika ujumbe wake kwa kanisa la Sardis, kanisa hili linaambiwa kwamba lilijiamini kupita kiasi kwamba liko salama kumbe lina hali mbaya. Linaambiwa likazane liendeleze kile kidogo kilichobaki nacho ili angalau lisipoteze kila kitu. Ujumbe huu unatuhusu na sisi pia. Hata sisi tunayochembe ya imani na wema ambayo bado ipo ndani yetu tuzidishe bidii angalau tuiwashe ili isizime kabisa. Hii ndio itakayotuokoa.
Hivyo bidii na kuonyesha nia ni kitu kitakachomuokoa mkristo. Lakini uzembe na kukata tamaa vitamuangusha. Sisi tuwe watu wa bidii. Pia katika ujumbe wake kwa kanisa la Laodicea, linalaumiwa kwa sababu lilikuwa vuguvugu-lilikuwa na unafiki mkubwa na lilichanganya mambo na kujiona liko salama kumbe liko kwenye hali mbaya na hivyo linashauriwa lije na kununua dhahabu toka kwa Mwenyezi ili litakaswe. Ni ujumbe tunaoambiwa na sisi ndugu zangu. Sisi ndio tunaochanganya mambo. Tunakwenda kanisani na kwa waganga, tunavaa rozari na hirizi kwenye mwili huu huu. Tunafanya uasherati tukiwa tumevaa hata rozari, tunalewa na bado tunajiita wakristo. Kweli Mungu atatutapika. Twende kwake tuombe hii dhahabu itutakase. Tuirudie sakramenti ya upatanisho nasi tutakuwa weupe tena.
Katika injili, Zakayo anatuonyesha mfano wa kuja kununua hii dhahabu safi toka kwa Yesu. Alipanda juu ili amuone na huu ukawa mwanzo wa uongofu wake kumfuata Yesu na akatakaswa kabisa na hata kuanza kutubu.
Sisi tuwe kama Zakayo, tupande juu na Yesu ataona bidii yetu na kuja kwetu. Tunapanda juu kwa kuungama na Yesu atakuja kwetu sasa na kushiriki karamu pamoja nasi kama iliyotokea kwa Zakayo. Ameni.
Maoni
Ingia utoe maoni