Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Oktoba 23, 2020

Ijumaa, Oktoba, 23, 2020,
Juma la 29 la Mwaka wa Kanisa

Ef 4:1-6;
Zab 23:1-6;
Lk 12:54-59


KUFAFANUA ALAMA ZA NYAKATI ZETU!


Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanza kwa kuiangalia zaburi yetu ya wimbo wa katikati ambapo tunakutana na zaburi yetu ikisitizia miongoni mwa mengine-juu ya mtu atakayeweza kupanda mlima wa Mungu. Inasema ni yule aliyena mikono safi asiyedhulumu.

Katika Biblia, Abrahamu, Musa na Elia ni miongoni mwa waliopanda mlima Mtakatifu wa Mungu na huko basi waliweza kukutana na Bwana na kuongea naye. Na kweli hawakuwa na mioyo ya kunyanyasa yeyote yule.

Huu ndio ujumbe ambao Paulo anawaachia wale Wakristo Waefeso leo kwamba nao basi wawe na moyo kama huu ili waupande mlima wa Bwana. Wasaidiane, wabebeane mizigo yao, kwa kujitolea, ukarimu na uvumilivu.

Huu ndio wito wetu kama wakristo. Hizi ndizo tunu tunazoalikwa kuzifufua kila kukicha kama wakristo. Wakristo tuzidishe uvumilivu na kujitolea. Uvumilivu na kujitolea umekosekana ndani ya jumuiya yetu siku hizi. Kila mmoja anatafuta chake, wengi wanaachwa bila matunzo kwa kukosekana watu wanaojitolea. Wengi wetu ni maskini siku hizi kwa sababu idadi kubwa hatujitolei. Tunahitaji watu wa kujitolea; tuijenge jumuiya yetu. Wengi wameshindwa kusoma au kupata ujuzi wowote kwa kukosekana wa kujitolea. Tunahitaji watu wenye kujitolea zaidi.

Katika injili Yesu anawaeleza makutano kwamba wao ni wataalamu sana kwa mambo ya kidunia, wanajua kutabiri mengi yahusuyo dunia lakini kuhusu nyakati za mwisho hawajui namna ya kuzitabiri. Yote haya yanatokea kwa sababu waliyatupa mambo haya ya Kimungu pembeni na wakaishia kutokujua zaidi juu ya nyakati za mwisho.

Hii itupatie changamoto hasa sisi tulio na ujuzi au kisomo fulani. Mara nyingi unakuta watu tunaujuzi fulani, tunajua biashara, mahesabu, kemia, kuendesha gari vizuri, kupasua watu kama daktari mzuri lakini inapotokea mambo ya Kimungu tupo hewa. Tubadilike, tujihusishe na mambo ya Kimungu, tusitumie muda wote kwa ajili ya mambo ya hapahapa tu duniani bila kutenga muda kwa ajili ya mambo ya Kimungu.

Kila mwenye ujuzi aangalie asitumie muda wote kwenye huo ujuzi wake. Aache pia muda kwa ajiili ya kuongea na Mungu ili basi amfundishe juu ya nyakati zijazo; atufundishe namna ya kutabiri majira na nyakati. Tusibakie wajinga

Maoni


Ingia utoe maoni