Jumatatu, Septemba 14, 2020
Jumatatu, Septemba 14, 2020,
Juma la 24, la Mwaka wa Kanisa
Sikukuu ya Kutukuka kwa Msalaba Mtakatifu
Hes 21: 4-9
Zab 77: 1-2, 34-38
Fil 2: 6-11
Yn 3: 13-17
MSALABA WA KRISTO NI TUMAINI NA UKOMBOZI WETU!
Karibuni ndugu zangu kwa adhimisho la Misa Takatifu. Ndugu zangu, leo tunaadhimisha sikuuu ya kutukuka kwa msalaba. Masomo yetu ya leo yanatuongoza vyema kwenye kutafakari sikukuu hii. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Hesabu. Hapa tunawakuta wana wa Israeli wanakosa Imani na kuanza kulalamika wakitaka kurudi Misri, wakale matango, matikiti maji, na mboga. Mungu anakasirika na kupeleka nyoka wa sumu wanao wauma na watu wengi kufa.
Wanamlilia Mungu naye Musa anapewa njia ya ajabu kidogo ya kuwaokoa-ajabu kabisa-kutengeneza nyoka wa shaba na kumwinua juu ya kamlingoti fulani halafu atakayemwangalia atapona tu, ataokoka tu. Kwa kweli hii ilikuwa ni njia yapkee kidogo-lakini Mungu anaitumia.
Injili Yesu anapozungumza na Nichodemus, tunapata maelezo ya kwa nini Mungu alitumia hii njia ambayo ni ya pekee-lengo lilikuwa kutabiri wokovu. Alitabiri juu ya Mwanae atakayetundikwa hivyo hivyo na kila atakayemwangalia, ataokoka tu.
Ulimwengu nyakati za Yesu ulikuwa kama hili jangwa la Sinai. Watu walikuwa wamekosa Imani, wanamlalamikia Mungu, wamechoka neema za Mungu-yaani chakula cha mbinguni-sasa wamesharudi Misri kula yale matango, matikiti maji, vitunguu-ambayo ni kama mataputapu tu-vitu kama ulevi, uasherati-ulafi, uonevu, majigambo-yote hayo ni matango yaliyoko Misri-umeshachoka kula ile mana-yaani sakramenti-unataka ukale matango-mataputapu, dhambi na ndiyo maana waliadhibiwa, watu walikuwa wameshaanza kufa kwa dhambi kama wana wa Israeli walivyokufa kwa kungatwa na nyoka.
Ulimwengu ukiwa katika mataputapu hayo, Mungu anamtuma Mwana wake anakufa msalabani na kila atakayemwangalia akiwa pale msalabani, ataokoka, ataponywa na sumu aliyopokea kutokana na kutamani au kula hayo matango au matikiti maji yake aliyokwenda kuhangaikia.
Hivyo sikukuu ya leo ni siku ya kumwangalia Yesu msalabani ili atuokoe na dhambi zetu. Ni siku ya kuhakikisha kwamba tunatumia vizuri zile sakramenti alizozitoa kwa ajili yetu wasafiri wa Jangwa la dunia. Usizichoke, usitamani matango kuliko mana na kuanza kulalamika ati Mkate ule ule kila siku, mbona hata hatubadilishiwi uwe na ladha fulani au na sukari-tupewe mkate mbadala bwana. Hapana! tusifanye hivyo, hapa Mungu ataamka na hasira na kutumaliza.
Sisi tuwe watu wa kushukuru. Tutumie vizuri sakramenti hizi alizotupa-watu hawazitaki kwa sababu hazivutii-lakini kumbuka Waisraeli walisema hivyohivyo juu ya mana wakiwa jangwani-wakidai imepoteza utamu-sisi tutumie sakramenti zote-na ndoa tufunge, na kitubio tufanye, Ekaristi tupokee-na wale vijana ambao hatujapokea kipaimara tupokee. Tusipozitumia sakramenti, nyoka wa sumu watatumaliza hapa jangwani-duniani.
Hivyo basi msalaba ndio nyoka yetu ile ya shaba. Tuutazame tupate kuponywa na nyoka waliotungata huku ulimwenguni. Kila mmoja amekwishangatwa na nyoka huku ulimwenguni kutokana na kiburi chake mbele ya Mungu. Wachunguze ni nyoka wapi wanaokungata na moja kwa moja nenda mbele ya msalaba nawe utapona. Tusipokwenda hakika hatupo salama.
Pia ni lazima nasi tukubali kuwa kama nyoka wa shaba kwa wengine, tuwe kama ishara ya msalaba kwa wengine. Kila anayekutazama, atoke na tumaini, aponywe na nyoka wanaomngata. Toa matumaini.
Maoni
Ingia utoe maoni