Jumapili, Agosti 09, 2020
Jumapili, Agosti 9 2020
Juma la 18 la Mwaka
1 Fal. 19:9, 11-13
Zab. 85 :8-13, (K)7
Rum 9: 1-5
Ml 14:22-33
Upo msemo usemao “bahari shwari haitoi wanamaji stadi.” Bahari yenye mawimbi mazito huwaimarisha wanamaji wake. Matatizo kama mawimbi yanaweza kukuimarisha. Tuwe tayari kuyapokea mawimbi yanayojitokeza ndani ya maisha yetu. Kuwa na mtazamo hasi dhidi ya matatizo ni kama kupambana na ukuta. “Wavuvi wanajua kuwa bahari ni hatari na ina dhoruba za kuogopesha, lakini hawajawahi kuona hatari hizi kama sababu tosha za kubaki kandokando ya bahari au ufukweni,” alisema Vincent van Goth. Wavuvi hujitosa kwenye maji marefu. Wavuvi ni mfano wa kuigwa tunapokumbana na mawimbi ya matatizo katika bahari ya maisha. Kuna mtu aliyemwambia mvuvi hivi: “wewe hauogopi kwenda baharini kuvua samaki? Mjomba wako, kaka yako na babu yako wote walikufa maji, kwa nini hauogopi?” Mvuvi alijibu hivi: “watu wengi hufa wakiwa vitandani lakini watu hawaachi kulala vitandani.” “Kuna mambo ambayo unajifunza vizuri sana wakati kuna utulivu na mengine wakati kuna dhoruba,” alisema Willa Cather
Kwa Yesu si kila mara mawingu yalibaki bluu. Kuna wakati wingu lilikuwa jeusi likiashiria dhoruba na matatizo. Alikataliwa na wasamaria katika kijiji cha Wasamaria (Lk 9:51-56). Pia kwa Ayubu mawingu hayakuwa kila mara ya bluu. Katikati ya mawimbi ya matatizo, Ayubu alizidi kuimarika. Ni kama jani la chai linapata nguvu ya kugeuza rangi ya maji likiwa kwenye maji moto. Ukiwa kwenye mawimbi ya matatizo kumbuka ukweli huu: Kwanza, tuko salama kwenye mawimbi ya matatizo tukiwa na Mungu kuliko tukiwa pasipokuwa na mawimbi ya matatizo bila Mungu. Mungu anaweza kutuliza mawimbi au akayaacha mawimbi akamtuliza binadamu. Pili, maisha bila mawimbi ya matatizo hufanya uwezekano wa mazuri kuwa sifuri. Tatu, tukumbuke kwamba joto likizidi, kutanuka kunazidi-matatizo makubwa yanaweza kukufanya uwe mkubwa. Kuna methali isemayo: “anayesema sijawahi kuliona jambo hili, si mkubwa kiumri.” Nne, ukiomba mvua inyeshe-kuwa tayari kukanyaga matope. Tano, tambua kwamba mawimbi ya matatizo yanakujia ili kukuimarisha na si kukudhoofisha.
Imani Haba
“Ewe mwenye imani haba mbona uliona shaka” (Mathayo 14:31)
Maisha ni kigeugeu. Mambo yalimgeuka mtume Petro. Petro alikuwa mtu wa kufanya maamuzi kwa ghafla na haraka. Hakufikiri sana kabla ya kutenda. Jambo hili pengine ni busara likilinganishwa na mtu ambaye anafikiri sana mwishowe hatendi lolote. Katika nafsi ya Petro, kuna mchanganyiko wa mambo. Anatamani kuwa na Yesu. Pia anatamani kuonesha kuwa anaweza kutenda analolitenda Yesu: kutembea juu ya maji. Kuna upendo na majivuno kama ilivyo kwa kila mmoja wetu. Petro ana ujasiri na woga. Anaanza vizuri, anaona dhoruba na kuogopa. Anakosa imani.
Sababu kubwa ya kupotea kwa imani ya Petro ni kwa kuwa macho yake, mawazo yake na moyo wake alivielekeza kwenye dhoruba badala ya Kristu. Alipomtazama Yesu Kristu, imani ilipatikana akalia kwa sauti, “ Bwana, niokoe!” (Mt 14; 30). Licha ya Petro kuwa na imani haba, Yesu alimuokoa. “Hapo, Yesu akanyosha mkono wake, akamshika … wakapanda mashuani, na upepo ukakoma” (Mt 14: 31-32). Nasi tunapambana na matatizo. Matatizo ya siku hizi ni kama: umasikini, makazi duni, ukosefu wa kazi, magonjwa yasiyo na tiba, ukosefu wa riziki, uzinifu, uzazi kwa namna isiyo halali, ukatili na vita, ukabila- damu inakuwa nzito kuliko maji ya ubatizo. Tumwombe Yesu atuokoe.
Katika kilele cha dhoruba, Yesu alijitokeza. Katika kilele cha hatari, katika upeo wa wasiwasi, Yesu alijitokeza. Anakuja wakati ambapo hategemewi kabisa. Mitume walifikiri ni mzuka wakauotea mbali. Yesu ni Mkombozi tunayeweza kumkimbilia. Alifanya kile ambacho binadamu hawezi kufanya. Alitembea juu ya maji. Vile ambavyo hatuwezi kufanya tumuachie yeye. Wakati tunapozama kwenye bahari ya matatizo, tulie kwa sauti: “Bwana utuokoe !” Shibisha imani yako na mashaka yako. Imani ikiongezeka, mashaka yanapungua na kinyume chake ni kweli. “Imani si kujaribu kuamini jambo bila ya kuzingatia ushahidi: imani ni kujaribu kufanya jambo bila kuzingatia matokeo,” alisema Sherwood Eddy. “Wanashinda wale wanaoamini wanaweza,” alisema Virgil. Ni katika mtazamo huo Erasmus alisema, “Amini kuwa unacho na unakuwa nacho.” Swali kubwa hapa si kuwa una imani au hauna imani. Jambo la msingi ni imani katika nini na imani katika nani. Ili kufanikiwa na kushinda, unahitaji kuwa na imani katika Mungu na kujiamini hata ikiwa imani ndogo au haba inatosha kukuondolea vikwazo, vihunzi na vizingiti. Tunasoma hivi katika Biblia, mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii” (Luka 17: 5-6).
Kifungu cha Biblia hicho kinabainisha ukweli huu, imani kidogo yaweza kufanya mambo makubwa. Ni ukweli unaoendana na ujumbe wa methali ya Kiswahili, “Kidogo kidogo kamba ukatika.” Nguvu ya mbegu haitegemei ukubwa au udogo wake inategemea uhai uliofichwa katika mbegu hiyo. Kuna nguvu ambayo imefichwa ndani mwako. Kama ni hivyo unahitaji kujiamini kuwa utaweza kufanikiwa katika maisha. Kwa imani na kujiamini ndege imevumbuliwa. Kwa imani na kujiamini, simu za mkononi zimegunduliwa. Kwa imani na kujiamini utalaamu wa kutengeneza runinga umefunuliwa.
Mitume walipoomba kuongezewa imani, Yesu hakusema nimewaongezea imani. Hakuahidi kuwaongezea imani. Ni kama aliwaambia anza na mlicho nacho, kidogo huvuta kikubwa, kidogo huzaa kikubwa, laini huzaa ngumu. Walikuwa kama mfanyabiashara asemaye nina pesa kidogo sana ngoja iwe nyingi ndipo nianze kufanya biashara. Je, itaongezekaje bila kuzalisha, kuuza na kununua? Walikuwa kama mkulima asemaye ‘nina mbegu lakini hazitoshi nitalima nikiwa na mbegu za kutosha.’ Anza na ulicho nacho. Hawezi kusema sina pesa yote ya kujenga na kumalizia nyumba. Anza kujenga na pesa uliyo nayo. Ili kuwa na zaidi, anza na ulicho nacho. Aliyenacho ataongezewa-ndivyo Bwana Yesu alivyofundisha.
Imani ni ufunguo wa mafanikio. Na sifa ya mtu anayefanikiwa ni kuwa ana imani. Imani kamili ndiyo kumtegemea Mungu na kumtumaini na kumtii. Tukiwa na imani kwa Mungu twaweza kusema, “Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa” (Waebrania 13:6). Hatuna budi kuwa na imani na uwezo Mungu aliotujalia yaani kujiamini. Kuna hadithi juu ya wakristu ambao walimuomba mchungaji wakati wa ibada ya Jumapili iliyokuwa inafuata waombe kupata mvua baada ya mvua kutonyesha kwa kipindi cha muda mrefu. Walishangaa siku hiyo ya maombi ya Jumapili mchungaji aliposema hayuko tayari kuomba kupata mvua maana watu hawaonyeshi imani kwa vile hawakwenda na miavuli ya kujikinga mvua. Imani lazima ionekane katika matendo. Mungu anasaidia na wewe unaweka juhudi na maarifa. Henry Ford alisema, “Kama unaamini unaweza kufanya jambo fulani au hauamini kama unaweza kufanya jambo fulani, uko sawa.” Usipoamini kwamba jambo fulani linaweza kufanyika, halitafanyika. Ukiamini, litafanyika. Imani inafukuza mashaka kama mwanga ufukuzavyo giza. Mashaka yakibisha hodi mlangoni mwako, itume imani-ijibu mashaka. Sala yetu iwe kama ya kijana mmoja kwenye Biblia, “Naamini, nisaidie kutokuamini kwangu” (Marko 9: 24).
Dunia ni bahari yenye mawimbi-inahitaji wanamaji stadi. Duniani kuna mengi sawasawa na bahari. Kuna papa na nyangumi tena wale wa hatari. Lakini ukweli unabaki: Bahari shwari haitoi wana maji stadi. Bahari iliyotulia haiwezi kuwatoa wanamaji hodari. Kuna methali ya Kiswahili isemayo: Bahari haishi zinge. Zinge ni machafuko ya mara kwa mara (mabadiliko ya ghafla). Bahari daima imo katika mabadiliko wala haitabiriki. Maisha kama vile bahari yamejawa na mema na maovu na yanapotujia sharti tuwe tayari kuyakabili. Tukabili mawimbi kwa utulivu bila hofu. Tukabili mawimbi ya mawazo mabaya, mahusiano mabaya na kushindwa.
Sala:
Ee Bwana ninakuomba unipe imani niweze kupambana na dhoruba za maisha nikitambua kwamba hakuna mawimbi yasiyokuwa na Mwisho,
Amina.
Maoni
Ingia utoe maoni