Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Juni 15, 2020

Jumatatu, Juni, 15, 2020,
Juma la 11 la mwaka

1 Fal 21: 1-16;
Zab 5: 2-3, 5-7;
Mt 5: 38-42

KUUSHINDA UOVU KWA WEMA!

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Mungu asubuhi ya leo. Leo tafakari yetu inaanzia katika zaburi ya wimbo wa katikati na hapa tunakutana na zaburi ya Daudi. Daudi akilia akimuomba Mungu asikilize ukelele wa sauti yake. Hii ni sala aliyoisali kwa nguvu sana alivyokuwa kazungukwa na hatari kubwa iliyotaka kuteketeza maisha yake. Miongoni mwa hatari kali zilizomzunguka Daudi, ni ile ya Sauli kuingia ndani ya pango alilokuwa kajificha na hivyo ama kweli Daudi alitetemeka sana kuona hili. Alivyokuwa kule ndani, hakika alisali sana kuomba Mungu ampe usalama dhidi ya adui huyu aliyekuwa na nguvu za kipesa, kijeshi na kifalme.

Lakini basi leo kwenye masomo yetu, anayelia ni Maskini mmoja aitwaye Nabothi. Yeye alikataa kuuza shamba la wazazi wake, shamba lililokuwa urithi kwake na lilikuwa na vitu kama makaburi ya wazazi wake. Na hivyo aliona ni aibu kwa kizazi chake chote kama angaliliuza shamba ili ati kwa sababu tajiri mmoja alitaka kutengeneza shamba la mizabibu. Tajiri huyu angaliweza kwenda kutengeneza shamba hili mahali pengine. Lakini basi yeye anakataa na hapohapo basi habari zinamfikia mke wa mfalme anayeamuru huyu Nabothi auawe na shamba kuchukuliwa. Nabothi alipokuwa anauawa, alitoa kilio kikali sana kwa Mungu kumwomba amsadie. Kilio hiki kweli kilijibiwa na Mungu kwani huyu Ahabu na yule mke wake walioamuru kifo cha huyu mtu, waliishia kupewa adhabu kali kabisa; jambo hili liliwafanya nao wapewe hukumu zilizogharimu maisha yao.

Ndugu zangu, kwa nyakati zetu tumeshuhudia wengi wakidhulumu sana. Kuna viongozi wanaopewa fedha za maendeleo ya nchi wanaishia kuzitapanya. Wengine wanapewa pesa za maendeleo ya shule au hospitali au kwenye kununua dawa za hospitali na wao wanazila. Wengine wanahamisha hata madawa ya hospitali kwenye pharmacy zao. Na tunawaona wanaofanya hivi kuwa ni wajanja wazuri sana.

Ndugu zangu, tuwe makini: tukumbuke kwamba kilio cha hawa wote wanaokosa huduma wakitulilia na hicho kilio kikitua mbele za Mungu, hakika tutaishia pabaya sana. Wengi tunalaaniwa kutokana na mambo kama haya. Dhuluma ni hatari. Kama baba kadhulumiwa na labda kafukuzwa kazini-na yeye akamlilia Mungu, na watoto wake na mke wake wakajiunga naye kumlilia Mungu, unafikiri kwamba aliyedhulumu atakuwa salama kweli? Jamani, tuache tabia hizi. Hizi ni laana. Wengi wetu tusiwe hivi.

Katika injili tunakutana na Yesu akitufundisha kwamba tusionyeshe jino kwa jino. Mtu akikupiga kofi shavu hili geuza na jingine. Yesu anapofundisha hivi sio kwamba anataka wanyonge waonewe Zaidi. Tujue kwamba hapa ndio atakavyoweza kushughulika vizuri na wale wanaonea wengine kama akina Ahabu na Mke wake. Tujue kwamba mtetezi wa wadogo ni Mungu. Hakika yeye atawatetea tu. Hivyo, tusiwadhulumu. Tumsifu Yesu Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni