Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Jumapili, Juni 14, 2020

Jumapili, Juni 14, 2020.
Juma la 11 la Mwaka wa Kanisa

Sherehe ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristu (Corpus Christi)

Kumb 8: 2-3, 14-16;
Zab 147;
1 Kor 10: 16-17;
Yn 6: 51-58.

EKARISTI-UJUMBE MKUBWA WA UPENDO WA NYAKATI ZOTE.

Sister Muagustiniani, sister Juliana wa Liège (Belgium) alipata maono ya kanisa likiwa chini ya mwezi unaongaa wenye kidoti kimoja cheusi. Doti hii ikionesha kutokuwepo kwa sherehe ya Ekaristi. Hii ilifanya baadaye kuwepo na sherehe ya Mwil na Damu ya Kristo ambayo iliwekwa kwenye kalenda ya Litirujia ya Kanisa mwaka 1264 chini ya Papa Urban wa IV. Je kulikuwa na haja ya kuwa na sherehe hii ya Ekaristi? Sherehe kama hii kawaida inatupa nafasi ya pekee ya kumshukuru Mungu kwa zawadi ya uwepo wa Kristo kuwa nasi daima, ambaye yupo kweli katika Ekaristi Takatifu. Kwa upande mwingine, ni wakati wetu wakutafakari fumbo hili kubwa la upendo. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ambayo ni kilele cha Sakramenti zote, ndani yake Sakramenti nyingine zote huadhimishwa, kwasababu ni “Fumbo la mafumbo yote” na “Taji la Sakrament zote” sakramenti zote zinavishwa taji na Ekaristi Takatifu. Katika Ekaristi Takatifu hatupokei tuu neema bali tunampokea Bwana wa Neema.

Ekaristi Takatifu ni kilele cha sala sote na kuabudu kwetu. Hakuna njia nyingine ya kuwasiliana na Mungu, yenye undani na ukuu zaidi ya Ekaristi Takatifu. Hapa watu wawili (mtoaji na mpokeaji) wanakuwa katika umoja wa kweli, (ndani yake, naye ndani mwako). Tunapaswa kusali mara nyingi katika hali zote na sehemu yeyote kwasababu sala hizi zinatufanya tuunganike na Bwana na kujenga umoja naye. Lakini kwakweli, hakuna sala yeyote inayotoa muunganiko mkuu zaidi ya Ekaristi Takatifu. Hakuna yeyote wala chochote kinachopaswa kutufanya tushindwe kuwa wamoja na Kristo, na kwa njia ya umoja huu tupate nguvu tunayohitaji katika maisha yetu.

Jumapili hii tumekuja pamoja kuadhimisha Ekaristi Takatifu kwa roho ya furaha na mapendo. Kwa bahati mbaya kuna baadhi ya Wakatoliki wengi ambao hawaioni Ekaristi Takatifu katika hali tena. Idadi ya Wakatoliki wanao shiriki adhimisho la Ekaristi jumapili, baadhi ya sehemu inashuka kila mara. Misa sio sehemu ya maonesho, hawapati kile wanachotaka, watu wanapenda kitu kipya kila wakati na tena pengine chenye mtizamo wanaotaka wao. Ni ajabu utakuta Misa zinazo hudhuriwa mara nyingi ni, Jumatano ya Majivu, Jumapili ya Matawi, Jumapili ya pasaka na Noeli kwasababu kuna vitu ninaongezwa ndani yake kwa mfano, matawi, majivu, mishumaa nk. Wengi wanategemea Padre aweke utani kwenye mahubiri ili afanye watu wachangamke, wengine wanataka kwaya waimbe vizuri sana kwa sauti zenye kupendeza na pengine wacheze sana kwa midundo ya kisasa zaidi, vifaa bora zaidi vya muziki, wengine wanataka wasomaji wenye sauti nzuri zakupendeza masikioni mwao, viti vizuri vya kukaa, taa zenye mwanga mzuri wa kupendeza na vifaa vizuri vya sauti. Kwa kweli, haya yote ni mitazamo na matarajio. Mbaya zaidi, pengine wapo pia baadhi ya makuhani wamenaswa kwenye mtego huu. Badala ya kuwapa watu anachosema Mungu, anawapa watu wanachopenda kusikia na kuona. Kwa matokeo haya, neno la Mungu halihubiriwi kiaminifu na katika unabii na maana halisi ya Uwepo wa Mungu inapotezwa. Kumekuwako na ile hali ya mlalo (mwanadamu kwa mwanadamu) na kuacha ile hali ya wima (Mungu kwenda kwa Mwanadamu) ya liturujia.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikti XVI alikuwa akisisitiza kila wakati kwamba “Liturjia ni Tendo la Mungu”. Hatupaswi kusahau kwamba kiini cha liturujia na maadhimisho ya Sakramenti ni Mungu na sio mwanadamu. Aliendelea pia kusema; “Katekesi nzuri juu ya Ekarisiti ni Ekaristi yenyewe ikiadhimishwa vizuri”. Kufahamu na kuamini kwamba Yesu yupo kweli katika adhimisho la Ekaristi, tunapaswa wote tufanye jitihada kufanya adhimisho hili lenye maana na furaha. Bila kusahau kwamba Ekaristi haiwi Ekaristi kwasababu ya Imani ya padre au Muumini. Baada ya sala ya Ekaristi (Konsekratsio) Yesu anakuwa kweli chini ya Maumbo ya mkate na divai. Uwe na Imani au usiwe na Imani, Yesu anabaki kuwa Yesu katika maumbo hayo daima. Tunadaiwa kuwa na Imani ili tuweze kushirikiana na neema ya Mungu lakini hata tusipokuwa nayo haimaanishi utamzuia Yesu kuwa katika maumbo hayo. Tushirikiane naye kwa Imani ili tupate neema.

Ni Mtakatifu Maximiliani Kolbe ambaye aliwahi kusema kwa hakika kwamba, “Utimilifu wa Misa sio wakati wa mageuzo bali ule umoja mtu anaoupokea wakati wa komunyo”. Tunaamini kwamba Ekaristi ni sadaka ile ile aliyo itoa Yesu pale msalabani na sio kumbukumbu ya kihistoria ya tukio lililopita, na kwamba mkate na divai unakuwa kweli mwili na damu ya Kristo, na pia tunaamini kwamba Ekaristi ni sakramenti ya Upendo wa Mungu kwetu. Sakramenti inayo adhimishwa katika Imani hiyo inatusaidia tuweze kuuona umoja wa ndani wa mtu na Mungu. “Wakati tunatazama Msalaba, unatambua ni kwajinsi ghani Yesu alitupenda, na ukitazama Ekaristi Takatifu unatambua ni kwa jinsi ghani Yesu ananipenda sasa” (Mt. Teresa wa Kolkota). Je, wakati tunautazama mkate wa uzima, tunatambua tunamtazama Mungu? Leo tunaalikwa tutafakari na kutambua sio tuu vipaji vya ajabu tulivyopewa bali tuangalie wema na unyenyekevu wa yule aliyejitoa mwenyewe.

Katika sherehe hii ya Mwili na Damu ya Bwana wetu Yesu Kristo, tufufue tena Imani yetu juu ya uwepo wa kweli wa Yesu katika Ekaristi Takatifu. Imani hii itujalie na kutusukuma kila wakati tuende kanisani kila jumapili tukiwa na furaha na hamu ya kukutana na Yesu ili maadhimisho ya Ekaristi yaweze kuwa yenye uhai na kweli nakuleta maana mbele ya Mungu. Kama kila wakati tutakuwa na haya mioyoni mwetu, itatusaidia kujitayarisha vyema- kimwili, kiakili na kiroho, ili tuweze kuadhimisha tukiwa wenye uchangamfu na kushiriki kikamilifu kwenye misa, nakumpokea Yesu katika komunyo Takatifu tukiwa tunastahili. Na hapo maadhimisho ya Ekaristi yataacha kuonekana kama tendo linalotuchosha nakuchukua muda wetu. Badala yake linakuwa kwetu kiini, chanzo na kilele cha maisha yetu kama Wakristo.

Sala:
ninakuabudu wewe Mungu uliye jificha kweli katika Ekaristi, katika maumbo ya mkate na divai. Moyo wangu wote unajikabidhi kwako, kwa kukutafakari wewe unajikabidhi kwako. Asante Bwana kwakungarisha maisha yangu kila siku kwa chakula cha malaika. Yesu, nakuamini wewe.
Amina.

Maoni


Ingia utoe maoni