Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Tafakari

Ijumaa, Mei 29, 2020

Ijumaa, Mei 29, 2020,
Juma la 7 la Pasaka

Mdo 25: 13-21;
Zab 103: 1-2, 11-12, 19-20 (K. 19);
Yn 21: 15-19.

JE, WANIPENDA?

Karibuni ndugu zangu kwa tafakari ya neno la Bwana katika siku ya leo tena. Bado tupo katika kipindi cha novena tukimuomba Roho Mtakatifu na hadi sasa naamini tumekwisha anza kusikia maisha yetu yakibarikiwa. Hivyo tuendelee kumwomba Roho Mtakatifu ili ifikapo ile siku ya pentekoste, angalau na sisi tuweze kufurahia yaliyowatokea mitume. Hili liwe ombi letu ndugu zangu. Na neno la Bwana leo katika somo la injili tunamkuta Yesu akiongea na Simoni Petro katika hisia kali. Anamuuliza mara tatu kama anampenda; anamueleza kwa hisia na msisitizo mkubwa sana. Anamuuliza je, wanipenda-basi tunza kondoo wangu. Kama nilivyokwishadokeza katika tafakari zilizopita, ni kwamba hapa Yesu alikuwa anataka kumpima Petro na kumweleza-je, kweli umekuwa rafiki kwangu? Wewe kweli ni rafiki yangu? Kama ni rafiki yangu ni lazima upende kile kilichomali yangu-yaani kondoo wangu. Hiki ndicho kipimo cha urafiki.

Mara nyingi mtumwa haonagi uchungu na kitu cha Bwana wake-yeye unaweza kumwambia akaoteshe mahindi lakini yeye ataotesha mahindi kumi kumi kwenye shimo moja. Ukimwambia akubebee labda mzigo wa gunia la mahindi akiona ni zito anaweza kulitoboa ili mahindi yamwagike njiani ili uzito upate kumpunguka. Lakini rafiki asingefanya hivyo. Rafiki atajitolea, kama ni mzigo mzito-ataona afadhali augawe mara mbili kuliko kuutoboa na mahindi kumwagika barabarani. Ndivyo ilivyo kwetu sisi ndgu zangu. Upendo wetu urafiki wetu na Yesu unaonekana kwa pale tuwapotayari kupenda kile anachokipenda Yesu.

Ndugu zangu, sisi kwa ubatizo wetu tuliahidi kuwa rafiki wa Yesu. Tuoneshe hili kwa kuwapenda kondoo wake. Yesu anategemea tukikutana na kondoo wake akiwa na njaa, au kiu au katika msongo wa mawazo tumfariji. Kumfariji kondoo hakuhitaji labda niwe na pesa ya kumpa bali nitambue kwamba hata kauli yangu nzuri yaweza kumfariji kondoo kwa namna ya ajabu. Tunatakiwa kuguswa kila tuonapo kondoo wa Yesu wakinyimwa uhai kwa utolewaji wa mimba, wengine wakiwa wamekumbwa na utapiamlo, wengine wakibebeshwa mimba katika umri mdogo, wengine wakijiingiza katika biashara ya uasherati-tusifurahie kuwaangalia miili yao. Tuone huruma. Kufurahia kuangalia miili ya kondoo hawa ni dalili ya roho ya muovu. Yote haya kama rafiki wa Yesu ni lazima yatuguse.

Katika somo la kwanza, tunakutana na Paulo akiendelea kushikiliwa kizuizini. Amefanya kazi yote ya kuhubiri injili lakini udhia anaoupata ndio huu. Tutambue kwamba Paulo aliweza kufikia hatua hii kwa sababu alielewa ukweli kwamba yeye ni rafiki wa Yesu. Hivyo alikuwa tayari kila wakati kuitetea injili ya Bwana na kondoo wa Bwana. Kwa tendo hili lake la kutoogopa vifungo au hata kifo au madhulumu, aliweza kuwatia moyo wale wakristo wa mwanzo na kuwawezesha nao waihubri injili bila kuogopa. Nasi tuepuke kuwa woga. Woga unawakwaza wale wanaokuja nyuma yako na mwisho wa siku kazi ya injili inashindwa kusonga mbele. Sisi kama askari walioko katika mstari wa mbele katika vita tuombe neema ya kuvumilia ili tuweze kutoa mfano kwa wale walio nyuma yetu. Sisi tulio mbele endapo tutakimbia basi kundi nzima nalo litarudi nyuma lote. Tuoneshe ujasiri na upendo wetu kwa Kristo.

Maoni


Ingia utoe maoni