Jumanne. 26 Novemba. 2024

Tafakari

Jumatatu, Oktoba 14, 2019

Jumatatu, Oktoba 14, 2019.
Juma la 28 la Mwaka

Rum 1: 1-7;
Zab 98: 1-4 (K) 2;
Lk 11: 29-32.


ISHARA YA YONA

Je, unatamani kwamba Mungu akupe ishara kutoka Mbinguni kama njia ya kukuonesha njia iliyo sawa au muelekeo mzuri wa maisha yako? Je, unategemea ishara kutoka kwa Mungu na kuitegemea? Kama Mungu alikuwa anatupa ishara ambayo inafunua kuhusu maisha yetu tungepaswa kuitegemea na kuipokea kama zawadi. Lakini kupokea ishara kutoka kwa Mungu ni tofauti na kutafuta ishara kutoka kwa Mungu.

Leo, Yesu anawaonya wale wanaotaka ishara. Kwa nini Yesu anaongea kwa ukali kuhusu kupinga ishara? Kwa sehemu kubwa, anataka sisi tumtafute yeye kwa njia ya Imani, badala ya ishara. Yesu anasema hakuna ishara mtakayopewa isipokuwa ishara ya Yona.

Ishara ya Yona ni ishara ya ufufuko. Sehemu ya kulinganisha inaoneshwa kwa zile siku tatu ambazo Yona alikaa ndani ya tumbo la samaki na kukaa kwa Yesu siku tatu katika tumbo la mama ardhi, na kufufuka siku ya tatu. Wote wawili Yona na Yesu walihubiri toba. Kuhubiri kwa Yona tu bila hata ya ishara ilitosha kabisa kwa watu wa Ninawi. Lakini, licha ya miujiza yote mikuu aliyofanya Yesu, haikutosha kwa watu kuamini kiasi kwamba wanahitaji tena ishara, kwa kweli mioyo ya Wayahudi ilikuwa migumu. Yesu anasema kwamba utume wake ni mkubwa hata kuliko ule wa Yona lakini ni ajabu kwamba watu wamekataa kutubu. Ndio maana Yesu anawaita kizazi kibaya na kilicho potoka, kwasababu hawaamini wala kuongoka. Yesu anahakikisha wafuasi wake wanamuelewa na kufahamu ufalme wake kwa uhakika.

Tafakari, juu ya “ishara” ambayo Mungu alishatoa. Na kama unajikuta mwenyewe ukihangaika na maswali ya maisha, geukia na kumbuka ishara ambayo Mungu alishakupa. Fungua macho na tazama kiini cha Imani yetu; uzima, kifo na ufufuko wa Yesu Kristo. Ni katika hili kila swali linapata jibu na kila neema inatolewa. Hatuhitaji kingine zaidi.

Sala:
Bwana, maisha yako, kifo na ufufuko ndio yote ninayo hitaji katika maisha yangu. Sadaka yako kamili inanipa mimi jibu kamili na kunipa kila neema. Ninakuomba nikugeukie wewe ishara ambayo ninahitaji kila siku. Yesu, nakuamini wewe.
Amina

Maoni


Ingia utoe maoni