Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. MONIKA (Jumatatu, Agosti 27, 2018)
The 1:1-5,11-12
Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo. Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi. Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili. Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa. Kwa hiyo twawaombea ninyi siku zote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kil ahaja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.
Zab. 96:1-5
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Mwimbieni Bwana, nchi yote.
Mwimbieni Bwana, libarikini jina lake.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake.
Tangazeni wokovu wake siku kwa siku.
Wahubirini mataifa habari za utukufu wake,
Na watu wote habari za maajabu yake.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake.
Kwa kuwa Bwana ni mkuu mwenye kusifiwa sana.
Na wa kuhofiwa kuliko miungu yote.
Maana miungu yote ya watu si kitu,
Lakini Bwana ndiye aliyezifanya mbingu.
(K) Wahubirini mataifa habari za utukufu wake, na watu wote habari za maajabu yake.
Zab. 147:12,15
Aleluya, aleluya,
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu, huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya.
Mt. 23:13-22
Yesu aliwaambia makutano na wafuasi wake: Ole wanu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnawafungia watu ufalme wa mbinguni; ninyi wenyewe hamwingii, wala wanaoingia hamwaachi waingie. Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnazunguka katika bahari na nchi kavu ili kumfanya mtu mmoja kuwa mwongofu; na akiisha kufanyika, mnamfanya kuwa mwana wa jehanumu mara mbili zaidi kuliko ninyi wenyewe. Ole wenu viongozi vipofu, ninyi msemao, Mtu atakayeapa kwa hekalu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa dhahabu ya hekalu, amejifunga. Wapumbavu ninyi na vipofu; maana ni ipi iliyo kubwa, ile dhahabu, au ile hekalu liitakasalo dhahabu? Tena, Mtu atakayeapa kwa madhabahu, si kitu; bali mtu atakayeapa kwa sadaka iliyo juu yake, amejifunga. Vipofu ninyi; maana ni ipi iliyo kubwa, ile sadaka, au ile madhabahu iitakasayo sadaka? Basi yeye aapaye kwa madhabahu, huapa kwa hiyo, na kwa vitu vyote vilivyo juu yake. Naye aapaye kwa hekalu, huapa kwa hilo, na kwa yeye akaaye ndani yake. Naye aapaye kwa mbingu, huapa kwa kiti cha enzi cha Mungu, na kwa yeye aketiye juu yake.
Maoni
Ingia utoe maoni