Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Bikira Maria Malkia (Jumatano, Agosti 22, 2018)  

Somo la 1

Isa. 9:2–7

Watu wale waliokwenda katika giza wameona nuru kuu; wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, nuru imewaangaza. Umeliongeza taifa, umezidisha furaha yao; wanafurahi mbele zako, kama furaha ya wakati wa mavuno, kama watu wafurahivyo wagawanyapo nyara. Kwa maana umeivunja nira ya mzigo wake, na gongo la bega lake yeye aliyemwonea, kama katika siku ya Midiani. Maana silaha zote za mtu mwenye silaha wakati wa mshindo, na mavazi yaliyofiringirishwa katika damu, yatakuwa tayari kuteketezwa, yatakuwa kuni za kutiwa motoni. Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa. Tumepewa mtoto mwanamume; na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake; naye ataitwa jina lake Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, Baba wa milele, Mfalme wa amani. Maongeo ya enzi yake na amani hayatakuwa na mwisho kamwe. Katika kiti cha enzi cha Daudi na ufalme wake; kuuthibitisha na kuutegemeza kwa hukumu na kwa haki, tangu sasa na hata milele. Wivu wa Bwana wa majeshi ndio utakaotenda hayo.

Wimbo wa Katikati

Zab. 113:1–8

Aleluya.
Enyi watumishi wa Bwana, sifuni,
Lisifuni jina la Bwana.
Jina la Bwana lihimidiwe
Tangu leo na hata milele.
(K) Jina la Bwana lihimidiwe tangu leo hata milele.

Toka maawio ya jua hata machweo yake
Jina la Bwana husifiwa.
Bwana ni mkuu juu ya mataifa yote,
Na utukufu wake ni juu ya mbingu.
(K) Jina la Bwana lihimidiwe tangu leo hata milele.

Ni nani aliye mfano wa Bwana,
Mungu wetu aketiye juu;
Anyenyekeaye kutazama,
Mbinguni na duniani?
(K) Jina la Bwana lihimidiwe tangu leo hata milele.

Injili

Lk. 1:26–38

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanawali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya maana gani? Malaika akamwambia, Usiogope. Mariamu kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Maoni


Ingia utoe maoni