Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 9 ya Mwaka (Jumatatu, Juni 04, 2018)  

Somo la 1

2Pet. 1:2-7

Neema na iwe kwenu na amani iongezwe katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu. Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika sabauri yenu utauwa, na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na ktika upendano wa ndugu, upendo.

Wimbo wa Katikati

Zab. 91:1-2, 14-16

Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Mungu wangu ninakutumaini.

Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, kw akuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nitamwitikia.
(K) Mungu wangu ninakutumaini.

Nitakuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza;
Kwa siku nyingi nitamshibisha,
Nami nitamwonyesha wokovu wangu.
(K) Mungu wangu ninakutumaini.

Shangilio

Zab. 130:5

Aleluya, aleluya.
Roho yangu inamngoja Bwana, na neno lake nimelitumainia.
Aleluya.

Injili

Mk. 12:1-12

Yesu alisema na Mafarisayo kwa mifano; Mtu mmoja alipanda shamba la mizabibu, akazungusha ugo, akachimba shimo la shinikizo, akajenga mnara, akapangisha wakulima, akasafiri. Hata kwa wakati wake akatuma, mtumwa kwa wale wakulima, ili apokee kwa wakulima katika matunda ya mizabibu. Wakamtwaa, wakampiga, wakamtoa nje, hana kitu. Akatuma tena kwao mtumwa mwingine, na huyo wakamtia jeraha -za kichwa, wakamfanyia jeuri. Akamtuma mwingine, huyo wakamwua; na wengine wengi, hawa wakiwapiga na hawa wakiwaua. Basi alikuwa na mmoja bado, mwana mpendwa wake; huyu naye akamtuma kwao mwisho, akisema, Watamstahi mwanangu. Lakini wale wakulima wakasemezana, Huyu ni mrithi; haya, na tumwue, na urithi utakuwa wetu. Wakamkamata, wakamwua, wakamtupa nje ya shamba la mizabibu. basi atafanyaje yule bwana wa shamba la mizabibu? Atakuja na kuwaangamiza wale wakulima, na lile shamba la mizabibu atawapa wengine. Hata andiko hili hamjalisoma, Jiwe walilolikataa waashi, hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni. Neno hili limetoka kwa Bwana, nalo ni ajabu machoni petu? Nao wakatafuta kumkamata, wakaogopa mkutano; maana walitambua ya kwamba ule mfano amewanenea wao. Wakamwacha wakaenda zao.

Maoni


Ingia utoe maoni