Masomo ya Misa
Dominika ya Matawi (Jumapili, Machi 25, 2018)
Isa 50:4-7
Bwana Mungu amenipa ulimi wa hao wafundishwao, nipate kujua jinsi ya kumtegemeza kwa maneno yeye aliyechoka, huniamsha asubuhi baada ya asubuhi; huniamsha, sikio langu lipate kusikia kama watu wafundishwao. Bwana Mungu amenizibua sikio langu, wala sikuwa mkaidi, wala sikurudi nyuma. Naliwatolea wapigao mgongo wangu, na wang'oao ndevu mashavu yangu; sikuficha uso wangu usipate fedheha na kutemewa mate. Maana Bwana Mungu atanisaidia; kwa sababu hiyo sikutahayari, kwa sababu hiyo nimekaza uso wangu kama gumegume, nami najua ya kuwa sitaona haya.
Zab 22:7-8; 16-19, 22-23
Wote wanionao hunicheka sana,
Hunifyonya, wakitikisa vichwa vyao;
Husema, Umtegemee Bwana; na amponye;
Na amwokoe sasa, maana apendezwa naye.
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha.
Kwa maana mbwa wamenizunguka;
Kusanyiko la waovu wamenisonga;
Wamenizua mikono na miguu.
Naweza kuihesabu mifupa yangu yote;
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha.
Wanagawanya nguo zangu,
Na vazi langu wanalipigia kura.
Nawe, Bwana, usiwe mbali,
Ee Nguvu zangu, fanya haraka kunisaidia.
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha.
Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu,
Katikati ya kusanyiko nitakusifu.
Ninyi mnaomcha Bwana, msifuni,
Enyi nyote mlio wazao wa Yakobo, mtukuzeni
(K) Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha.
Flp 2:6-11
Yesu mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu; tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina; ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi; na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristu ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
Flp 2:8-9
Kristu alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba. Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
Mk 14:1-15:47
Baada ya siku mbili ilikuwa sikukuu ya Pasaka, na mikate isiyochachwa; wakuu wa makuhani na waandishi wakatafuta njia ya kumkamata kwa hila na kumwua. Kwa maana walisema, Isiwe kwa wakati wa sikukuu, isije ikatokea ghasia katika watu. Naye alipokuwapo Bethania, nyumbani mwa Simoni mkoma, ameketi chakulani, alikuja mwanamke mwenye kibweta cha marhamu ya nardo safi ya thamani nyingi; akakivunja kibweta akaimimina kichwani pake. Palikuwa na watu waliochukizwa katika nafsi zao wakisema, Kwani kupoteza marhamu namna hii? Maana marhamu hii ingaliweza kuuzwa kwa dinari mia tatu na kuzidi, wakapewa maskini. Wakamnung'unikia sana yule mwanamke. Yesu akasema, Mwacheni; mbona mnamtaabisha? Amenitendea kazi njema; maana sikuzote mnao maskini pamoja nanyi, na kila mpendapo mwaweza kuwatendea mema; lakini mimi hamnami sikuzote. Ametenda alivyoweza; ametangulia kuupaka mwili wangu marhamu kwa ajili ya maziko. Amin, nawaambia, Kila ihubiriwapo Injili katika ulimwengu wote, na hili alilotenda huyu litatajwa kwa kumbukumbu lake. Yuda Iskariote, yule mmoja katika wale Thenashara, akaenda zake kwa wakuu wa makuhani, apate kumsaliti kwao. Nao waliposikia walifurahi, wakaahidi kumpa fedha. Akatafuta njia ya kumsaliti wakati wa kufaa. Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka? Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni; na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu? Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni. Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka. Basi ilipokuwa jioni yuaja pamoja na wale Thenashara. Nao walipokuwa wameketi chakulani, wakila, Yesu alisema, Amin, nawaambia, Mmoja wenu, naye anakula pamoja nami, atanisaliti. Wakaanza kuhuzunika, wakamwambia mmoja mmoja, Je! Ni mimi? Akawaambia, Ni mmoja wa hao Thenashara, ambaye achovya pamoja nami katika kombe. Kwa maana Mwana wa Adamu aenda zake kama alivyoandikiwa; lakini ole wake mtu yule ambaye amsaliti Mwana wa Adamu; ingekuwa heri kwake mtu yule kama asingalizaliwa. Nao walipokuwa wakila, alitwaa mkate, akabariki, akaumega, akawapa, akasema, Twaeni; huu ndio mwili wangu. Akatwaa kikombe, akashukuru, akawapa; wakakinywea wote. Akawaambia, Hii ndiyo damu yangu ya agano, imwagikayo kwa ajili ya wengi. Amin, nawaambia ninyi, Sitakunywa tena kabisa uzao wa mzabibu, hata siku ile nitakapounywa mpya katika ufalme wa Mungu. Nao walipokwisha kuimba walitoka kwenda mlima wa Mizeituni. Yesu akawaambia, Mtakunguwazwa ninyi nyote kwa ajili yangu usiku huu; kwa kuwa imeandikwa, Nitampiga mchungaji, na kondoo watatawanyika. Lakini baada ya kufufuka kwangu, nitawatangulia kwenda Galilaya. Petro akamwambia, Hata wajapokunguwazwa wote, lakini siyo mimi. Yesu akamwambia, Amin, nakuambia wewe, Leo, usiku huu, kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Naye akazidi sana kusema, Ijaponipasa kufa nawe, hata hivyo sitakukana kamwe. Na wote wakasema vile vile. Kisha wakaja mpaka bustani iitwayo Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa muda niombapo. Akamtwaa Petro na Yakobo na Yohana pamoja naye, akaanza kufadhaika sana na kuhangaika. Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe. Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe. Akaja akawakuta wamelala usingizi, akamwambia Petro, Je! Simoni, umelala? Hukuweza kukesha saa moja? Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu. Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo. Akaja tena akawakuta wamelala, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu. Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi. Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia. Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee. Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; mkamateni, mkamchukue salama. Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu. Wakanyosha mikono yao wakamkamata. Na mmoja wao waliokuwapo akafuta upanga, akampiga mtumwa wa Kuhani Mkuu, akamkata sikio. Yesu akajibu, akawaambia, Je! Ni kama juu ya mnyang'anyi mmetoka wenye panga na marungu, kunitwaa mimi? Kila siku nalikuwa mbele yenu hekaluni nikifundisha, msinikamate; lakini haya yamekuwa ili maandiko yapate kutimia. Ndipo wakamwacha, wakakimbia wote. Na kijana mmoja alimfuata, amejitanda mwili wake nguo ya kitani; wakamkamata; naye akaiacha ile nguo ya kitani, akakimbia yu uchi. Nao wakamchukua Yesu kwa Kuhani Mkuu; wakamkusanyikia wote, wakuu wa makuhani na wazee na waandishi. Naye Petro akamfuata kwa mbali, hata ndani katika behewa ya Kuhani Mkuu; akawa ameketi pamoja na watumishi, anakota moto mwangani. Basi wakuu wa makuhani na baraza yote wakatafuta ushuhuda juu ya Yesu wapate kumwua; wasione. Kwa maana wengi walimshuhudia uongo, walakini ushuhuda wao haukupatana. Hata wengine wakasimama, wakamshuhudia uongo, wakisema, Sisi tulimsikia akisema, Mimi nitalivunja hekalu hili lililofanyika kwa mikono, na katika siku tatu nitajenga jingine lisilofanyika kwa mikono. Wala hata hivi ushuhuda wao haukupatana. Kisha Kuhani Mkuu akasimama katikati, akamwuliza Yesu, akisema, Hujibu neno? Hawa wanakushuhudia nini? Lakini akanyamaza, wala hakujibu neno. Kuhani Mkuu akamwuliza tena, akamwambia, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wake Mtukufu? Yesu akasema, Mimi ndiye, nanyi mtamwona Mwana wa Adamu ameketi mkono wa kuume wa nguvu, akija na mawingu ya mbinguni. Kuhani Mkuu akararua nguo zake, akisema, Tuna haja gani tena ya mashahidi? Mmesikia kufuru yake; mwaonaje ninyi? Wote wakamhukumu kuwa imempasa kuuawa. Wengine wakaanza kumtemea mate, wakamfunika uso, na kumpiga makonde, na kumwambia, tabiri. Hata watumishi nao wakampiga makofi. Na Petro alikuwa chini behewani; akaja mmoja wa vijakazi wa Kuhani Mkuu, akamwona Petro akikota moto; akamkazia macho, akasema, Wewe nawe ulikuwapo pamoja na yule Mnazareti, Yesu. Akakana, akasema, Sijui wala sisikii unayoyasema wewe. Akatoka nje hata ukumbini; jogoo akawika. Na yule kijakazi akamwona tena, akaanza tena kuwaambia waliosimama pale, Huyu ni mmoja wao. Akakana tena. Kitambo kidogo tena wale waliosimama pale wakamwambia Petro, Hakika u mmoja wao, kwa sababu u Mgalilaya wewe. Akaanza kulaani na kuapiza, Simjui mtu huyu mnayemnena. Na mara jogoo akawika mara ya pili. Petro akalikumbuka lile neno aliloambiwa na Yesu, Kabla ya kuwika jogoo mara mbili, utanikana mara tatu. Na alipolifikiri, akalia. Mara kulipokuwa asubuhi wakuu wa makuhani walifanya shauri pamoja na wazee na waandishi na baraza nzima, wakamfunga Yesu, wakamchukua, wakamleta mbele ya Pilato. Pilato akamwuliza, Wewe ndiwe mfalme wa Wayahudi? Akajibu, akamwambia, Wewe wasema. Nao wakuu wa makuhani walikuwa wakimshitaki mambo mengi. Pilato akamwuliza tena akisema, Hujibu neno? Tazama ni mambo mangapi wanayokushitaki! Wala Yesu hakujibu neno tena, hata Pilato akastaajabu. Basi wakati wa sikukuu huwafungulia mfungwa mmoja, wamwombaye. Palikuwa na mtu aitwaye Baraba, amefungwa pamoja na watu waliofanya fitina, na kufanya uuaji katika fitina ile. Makutano wakaja, wakaanza kuomba awafanyie kama vile alivyozoea. Pilato akawajibu, akisema, Je! Mnataka niwafungulie mfalme wa Wayahudi? Kwa maana alitambua ya kuwa wakuu wa makuhani wamemtoa kwa husuda. Lakini wakuu wa makuhani wakawataharakisha makutano, kwamba afadhali awafungulie Baraba. Pilato akajibu tena akawaambia, Basi nimtendeje huyu mnayemnena kuwa ni mfalme wa Wayahudi? Wakapiga kelele tena, Msulibishe. Pilato akawaambia, Kwani, ni ubaya gani alioutenda? Wakazidi sana kupiga kelele, Msulibishe. Pilato akipenda kuwaridhisha makutano, akawafungulia Baraba; akamtoa Yesu, baada ya kumpiga mijeledi, ili asulibiwe. Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima. Wakamvika vazi la rangi ya zambarau, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani; wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi! Wakampiga mwanzi wa kichwa, wakamtemea mate, wakapiga magoti, wakamsujudia. Hata wakiisha kumdhihaki, wakamvua lile vazi la rangi ya zambarau, wakamvika mavazi yake mwenyewe; wakamchukua nje ili wamsulibishe. Wakamshurutisha mtu aliyekuwa akipita, akitoka mashamba, Simoni Mkirene, baba yao Iskanda na Rufo, ili auchukue msalaba wake. Wakamleta mpaka mahali paitwapo Golgotha, yaani, Fuvu la kichwa. Wakampa mvinyo iliyotiwa manemane, asiipokee. Wakamsulibisha, wakagawa mavazi yake, wakayapigia kura kila mtu atwae nini. Basi ilikuwa saa tatu, nao wakamsulibisha. Palikuwa na anwani ya mashitaka yake iliyoandikwa juu, MFALME WA WAYAHUDI. Na pamoja naye walisulibisha wanyang'anyi wawili, mmoja mkono wake wa kuume na mmoja mkono wake wa kushoto. [ Basi andiko likatimizwa linenalo, Alihesabiwa pamoja na waasi.] Nao waliokuwa wakipita njiani wakamtukana, wakitikisa-tikisa vichwa, wakisema, Ahaa! Wewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga katika siku tatu, jiponye nafsi yako, ushuke msalabani. Kadhalika na wakuu wa makuhani wakamdhihaki wao kwa wao, pamoja na waandishi, wakisema, Aliponya wengine; hawezi kujiponya mwenyewe. Kristo, mfalme wa Israeli, na ashuke sasa msalabani tupate kuona na kuamini. Hata wale waliosulibiwa pamoja naye wakamfyolea. Na ilipokuwa saa sita, palikuwa na giza juu ya nchi yote, hata saa tisa. Na saa tisa Yesu akapaza sauti yake kwa nguvu, Eloi, Eloi, lama sabakthani? Maana yake, Mungu wangu, Mungu wangu, mbona umeniacha? Na baadhi yao waliosimama pale, walisema, Tazama, anamwita Eliya. Na mmoja akaenda mbio, akajaza sifongo siki, akaitia juu ya mwanzi, akamnywesha, akisema, Acheni, na tuone kwamba Eliya anakuja kumtelemsha. Naye Yesu akatoa sauti kuu, akakata roho. Pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini. Basi yule akida, aliyesimama hapo akimwelekea, alipoona ya kuwa alikata roho jinsi hii, akasema, Hakika mtu huyu alikuwa Mwana wa Mungu. Palikuwako na wanawake wakitazama kwa mbali; miongoni mwao alikuwamo Mariamu Magdalene, na Mariamu mama yao Yakobo mdogo na Yose, na Salome; hao ndio waliofuatana naye huko Galilaya, na kumtumikia; na wengine wengi waliopanda pamoja naye mpaka Yerusalemu. Hata ikiisha kuwa jioni, kwa sababu ni Maandalio, ndiyo siku iliyo kabla ya sabato, akaenda Yusufu, mtu wa Arimathaya, mstahiki, mtu wa baraza ya mashauri, naye mwenyewe anautazamia ufalme wa Mungu; akafanya ujasiri, akaingia mbele ya Pilato akauomba mwili wake Yesu. Lakini Pilato akastaajabu, kwamba amekwisha kufa. Akamwita yule akida, akamwuliza kwamba amekufa kitambo. Hata alipokwisha kupata hakika kwa yule akida, alimpa Yusufu yule maiti. Naye akanunua sanda ya kitani, akamtelemsha, akamfungia ile sanda, akamweka katika kaburi lililochongwa mwambani; akavingirisha jiwe mbele ya mlango wa kaburi. Nao Mariamu Magdalene na Mariamu mamaye Yose wakapatazama mahali alipowekwa.
Maoni
Ingia utoe maoni