Masomo ya Misa
Jumamosi ya 34 ya Mwaka (Jumamosi, Desemba 02, 2017)
Dan. 7:15-27
Mimi Danieli, roho yangu ilihuzunika mwilini mwangu, na hayo maono ya kichwa changu yakanifadhaisha. Nikamkaribia mmoja wa hao waliosimama karibu, nikamwuliza maana ya kweli ya hayo yote. Basi akaniambia, akanijulisha tafsiri ya mambo hayo. Wanyama hao wakubwa walio wanne ni wafalme wane watakaotokea duniani. Lakini watakatifu wake Aliye juu wataupokea ufalme, na kuumiliki huo ufalme milele, naam hata milele na milele.
Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wanne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake. Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; hata akaja huyo mzee wa siku, nao watakatifu wake. Aliye juu wakapewa hukumu; na majira yakawadia watakatifu waumiliki ufalme.
Akanena hivi, Huyo mnyama wanne atakuwa ni ufalme wa nne juu ya dunia, utakaokuwa mbali na falme zile zote, nao utakula dunia yote, na kuikanyaga, na kuivunja vipande vipande. Na habari za zile pembe kumi katika ufalme huo wataondoka wafalme kumi; na mwingine ataondoka baada ya hao; naye atakuwa mbali na hao wa kwanza; naye atawashusha wafalme watatu. Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa wakati, na nyakati mbili, na nusu wakati. Lakini hukumu itawekwa, nao watamwondolea mamlaka yake, kuyapoteza na kuyaangamiza, hata milele. Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.
Dan. 3:82-87
Wanadamu, mhimidi Bwana;
Msifuni na kumwadhisha milele.
Bani Israeli, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na mwadhimisha milele.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Watumishi wa Bwana mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na mwadhimisha milele.
Roho na nafsi zao wenye haki mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni,
Mhimidini Bwana;
Msifuni na kumwadhimisha milele.
(K) Msifuni na mwadhimisha milele.
Yak. 1:18
Aleluya, aleluya,
Kwa kupenda kwake mwenyewe, Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli, tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya.
Lk. 21:34-36
Yesu aliwambia wanafunzi wake: Jiangalieni, mioyo yenu isije ikalemewa na ulafi, na ulevi, na masumbufu ya maisha haya; siku ile ikawajia ghafula, kama mtego unasavyo; kwa kuwa ndivyo itakavyowajilia watu wote wakaao juu ya uso wa dunia nzima. Basi, kesheni ninyi kila wakati, mkiomba, ili mpate kuokoka katika hayo yote yatakayotokea, na kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Maoni
Ingia utoe maoni