Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Kutabarukiwa Basilika la Laterani (Alhamisi, Novemba 09, 2017)  

Somo la 1

Eze 43:1-2, 4-7

Malaika alinileta mpaka langoni, yaani, lango lile lielekealo upande wa mashariki; na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulitokea kwa njia ya mashariki; na sauti yake ilikuwa kama mshindo wa maji mengi, nayo nchi iling'aa kwa utukufu wake. Na huo utukufu wa Bwana ukaingia ndani ya nyumba, kwa njia ya lango lile lielekealo upande wa mashariki. Kisha Roho ikaniinua, ikanichukua mpaka ua wa ndani; na tazama, utukufu wa Bwana uliijaza nyumba. Nikasikia sauti ya mmoja asemaye nami, itokayo katika nyumba hiyo; na mtu akasimama karibu nami. Akaniambia, Mwanadamu, hapa ni mahali pa kiti changu cha enzi, na mahali pa nyayo za miguu yangu, nitakapokaa kati ya wana wa Israeli milele

Wimbo wa Katikati

Zab 84:2-5, 11

Nafsi yangu imezionea shauku nyua za Bwana, 

Naam, na kuzikondea. 

Moyo wangu na mwili wangu Vinamlilia Mungu aliye hai. 

(K) Maskani zako zapendeza kama nini Ee Bwana wa majeshi


Shomoro naye ameona nyumba, Na mbayuwayu amejipatia kioto, 

Alipoweka makinda yake, Kwenye madhabahu zako, 

Ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu. 

Heri wakaao nyumbani mwako, Wanakuhimidi daima. 

(K) Maskani zako zapendeza kama nini Ee Bwana wa majeshi


Heri ambaye nguvu zake zatoka kwako, 

Na njia ziendazo Sayuni zimo moyoni mwake. 

Kwa kuwa Bwana, Mungu, ni jua na ngao, Bwana atatoa neema na utukufu. 

Hatawanyima kitu chema Hao waendao kwa ukamilifu.

(K) Maskani zako zapendeza kama nini Ee Bwana wa majeshi

Somo la 2

1Kor 3:9-13, 16-17

Ninyi ni shamba la Mungu, ni jengo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, Yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi. 


Injili

Yn 2:13-22

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu akakwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng'ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng'ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, nami katika siku tatu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu. 


Maoni


Ingia utoe maoni