Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Bikira Maria Mtakatifu wa Rozari (Jumamosi, Oktoba 07, 2017)  

Somo la 1

Mdo. 1:12-14

Yesu alipokwisha kupanda mbinguni mitume walirudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato. Hata walipoingia, wakapanda orofani, walipokuwa wakikaa; Petro, na Yohane, na Yakobo, na, Andrea, Filipo na Tomaso, Bartholomayo na Mathayo, Yakobo wa Alfayo, na Simoni Zelote, na Yuda wa Yakobo. Hawa wote walikuwa wakidumu kwa moyo mmoja katika kusali, pamoja nao wanawake, na Mariamu mama yake Yesu, na ndugu zake.    

Wimbo wa Katikati

Lk. 1:46-55

Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,

Na roho yangu imemfurahia Mungu, 

Mwokozi wangu.

(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.


Kwa kuwa ameutazama 

Unyonge wa mjakazi wake.

Kwa maana, tazama, tokea sasa

Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;

Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,

Na jina lake ni takatifu. 

(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.


Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi

Kwa hao wanaomcha.

Amefanya nguvu kwa mkono wake;

Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; 

(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.


Amewaangusha wakuu katika viti vyao vya enzi;

Na wanyonge amewakweza.

Wenye njaa amewashibisha mema,

Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. 

(K) Mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu.

Shangilio

Lk. 1:28

Aleluya, aleluya,

Salamu, uliyepewa neema, Bwana yu pamoja nawe. Umebarikiwa katika wanawake.

Aleluya.

Injili

Lk. 1:26-38

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani mwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe.

Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu ataitwa Mwana wa Aliye juu, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho.

Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu.

Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.


Maoni


Ingia utoe maoni