Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Kumbukumbu ya Malaika Walinzi (Jumatatu, Oktoba 02, 2017)  

Somo la 1

Kut. 23:20-23

Bwana asema hivi: Tazama, mimi namtuma malaika aende mbele yako, ili akulinde njiani na kukupeleka mpaka mahali pale nilipokutengezea. Jitunzeni mbele yake, mwisikize sauti yake; wala msimtie kasirani; maana, hatawasamehe makossa yenu; kwa kuwa jina langu limo ndani yake. Lakini ukiisikiza sauti yake kweli, na kuyatenda yote ninenayo mimi; ndipo mimi nitakuwa ni adui wa adui zako, na mtesi wa hao wakutesao. Kwa kuwa malaika wangu atatangulia mbele yako, na kukufikisha kwenye Mwamori, na Mhiti, na Mpezi, na Mkanaani, na Mhivi, na Myebusi; name nitawakatilia mbali.

Wimbo wa Katikati

Zab. 91:1-6.10-11

Aketiye mahali pa siri pake aliye juu,

Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.

Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,

Mungu wangu nitakayemtumaini. 

(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.


Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,

Na katika tauni iharibuyo.

Kwa manyoya yake atakufunika,

Chini ya mbawa zake utapata kimbilio. 

(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.


Hutaogopa hofu ya usiku,

Wala mshale urukao mchana,

Wala tauni ipitayo gizani.

Wala uele uharibuo adhuhuri, 

(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.


Mabaya hayatakupata wewe,

Wala tauni haitaikaribia hema yako.

Kwa kuwa atakuagizia malaika zake

Wakulinde katika njia zako zote. 

(K) Amekuagizia malaika zake wakulinde katika njia zako zote.


Shangilio

Mt. 18:1-5,10

Aleluya, aleluya,
Mhimidini Bwana, enyi majeshi yake yote, ninyi watumishi wake mfanyao mapenzi yake.
Aleluya.

Injili

Mt. 18:1-5.10

Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni.

Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi.

Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni.

Maoni


Ingia utoe maoni