Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne 5 ya Kwaresima (Jumanne, Machi 15, 2016)  

Somo la 1

Hes 21:4-9

Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia. Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu. Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa. Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu. Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Wimbo wa Katikati

Zab 102:1-2, 15-20


Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.
Usinifiche uso wako siku ya shida yangu, Unitegee sikio lako, siku niitapo unijibu upesi.
(K)Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.


Kisha mataifa wataliogopa jina la Bwana, Na wafalme wote wa dunia utukufu wako;
Bwana atakapokuwa ameijenga Sayuni, Atakapoonekana katika utukufu wake,
(K)Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.

Atakapoyaelekea maombi yake aliye mkiwa, Asiyadharau maombi yao.
Kizazi kitakachokuja kitaandikiwa hayo, Na watu watakaoumbwa watamsifu Bwana.
(K)Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.

Maana ametazama toka patakatifu pake pa juu, Toka mbinguni Bwana ameiangalia nchi,
Ili akusikie kuugua kwake aliyefungwa, Na kuwafungua walioandikiwa kufa.
(K)Ee Bwana, usikie kuomba kwangu, Kilio changu kikufikie.

Injili

Yn 8:21-30

Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; nanyi mtakufa katika dhambi yenu; mimi niendako ninyi hamwezi kuja. Basi Wayahudi wakasema, Je! Atajiua! Kwa kuwa asema, Mimi niendako ninyi hamwezi kuja? Akawaambia, Ninyi ni wa chini, mimi ni wa juu; ninyi ni wa ulimwengu huu, mimi si wa ulimwengu huu. Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu. Basi wakamwambia, U nani wewe? Yesu akawaambia, Hasa neno lilo hilo ninalowaambia. Ninayo mengi ya kusema na kuhukumu juu yenu; lakini yeye aliyenipeleka ni kweli, nami niliyoyasikia kwake, ndiyo ninenayo katika ulimwengu. Wala hawakutambua ya kuwa anawatajia Baba. Basi Yesu akawaambia, Mtakapokuwa mmekwisha kumwinua Mwana wa Adamu, ndipo mtakapofahamu ya kuwa mimi ndiye; na ya kuwa sifanyi neno kwa nafsi yangu, ila kama Baba alivyonifundisha ndivyo ninenavyo. Naye aliyenipeleka yu pamoja nami, hakuniacha peke yangu; kwa sababu nafanya sikuzote yale yampendezayo. Naye alipokuwa akisema hayo, wengi walimwamini.

Maoni


Ingia utoe maoni