Alhamisi. 02 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 5 ya Kwaresima (Ijumaa, Aprili 07, 2017)  

Somo la 1

Yer 20:10-13

Nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki; huenda akahadaika; nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake. Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe. Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu. Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; kwa maana ameiponya roho ya mhitaji katika mikono ya watu watendao maovu.

Wimbo wa Katikati

Zab. 18:1-6

Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu,
Mungu wangu, mwamba wangu ninayemkimbilia,
Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa,
Hivyo nitaokoka na adui zangu.
(K) Katika shida yangu nalimwita Bwana, akaisikia sauti yangu.

Kamba za mauti zilinizunguka,
Mafuriko ya uovu yakanitia hofu.
Kamba za kuzimu zilinizunguka,
Mitego ya mauti ikanikabili.
(K) Katika shida yangu nalimwita Bwana, akaisikia sauti yangu.

Katika shida yangu nalimwita Bwana,
Na kumlalamikia Mungu wangu.
Akaisikia sauti yangu hekaluni mwake,
Kilio change kikaingia masikioni mwake.
(K) Katika shida yangu nalimwita Bwana, akaisikia sauti yangu.

Shangilio

Shangilio

Mbegu ni neno la Mungu, mpanzi lakini ni Kristu, yeyote ampataye, ataishi milele.

Injili

Yn. 10:31-42

Wayahudi waliokota mawe ili wampige. Yesu akawajibu, Kazi njema nyingi nimewaonyesha zitokazo kwa Baba; kwa ajili ya kazi ipi katika hizo mnanipiga kwa mawe? Wayahudi wakamjibu, Kwa ajili ya kazi njema hatukupigi kwa mawe; bali kwa kukufuru, na kwa sababu wewe uliye mwanadamu wajifanya mwenyewe u Mungu. Yesu akawajibu, Je! Haikuandikwa katika torati yenu ya kwamba, Mimi nimesema, Ndinyi miungu? Ikiwa aliwaita miungu wale waliojiliwa na neno la Mungu; (na maandiko hayawezi kutanguka); je! Yeye ambaye Baba alimtakasa, akamtuma ulimwenguni, ninyi mnamwambia, Unakufuru; kwa sababu nalisema, Mimi ni Mwana wa Mungu? Kama sizitendi kazi za Baba yangu, msiniamini; lakini nikizitenda, ijapokuwa hamniamini mimi, ziaminini zile kazi; mpate kujua na kufahamu ya kuwa Baba yu ndani yangu, nami ni ndani ya Baba. Wakatafuta tena kumkamata; lakini akatoka mikononi mwao. Akaenda zake tena ng’ambo ya Yordani, mpaka mahali pale alipokuwapo Yohane akibatiza hapo kwanza, akakaa huko. Na watu wengi wakamwendea, wakasema, Yohane kweli hakufanya ishara yoyote, lakini yote aliyoyasema Yohane katika habari zake huyu yalikuwa kweli. Nao wengi wakamwamini huko.

Maoni


Ingia utoe maoni