Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 2 ya Mwaka (Jumapili, Januari 15, 2017)  

Somo la 1

Isa 49:3,5-6

Bwana aliniambia; Wewe u mtumishi wangu, Israeli, ambaye katika wewe nitatukuzwa.Na sasa Bwana asema hivi, yeye aliyeniumba tangu tumboni niwe mtumishi wake, ili nimletee Yakobo tena, na Israeli wakusanyike mbele zake tena; (maana mimi nimepata heshima mbele ya macho ya Bwana, na Mungu wangu amekuwa nguvu zangu); naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe nuru ya mataifa, upate kuwa wokovu wangu hata miisho ya dunia.

Wimbo wa Katikati

Zab 40:1, 3, 6-9

Nalimngoja Bwana kwa saburi,
Akaniinamia akakisikia kilio changu.
Akatia wimbo mpya kinywani mwangu,
Ndio sifa zake Mungu wetu.
(K) Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, Kuyafanya mapenzi yako.

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja,
(K) Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, Kuyafanya mapenzi yako.

Katika gombo la chuo nimeandikiwa,
Kuyafanya mapenzi yako, Ee Mungu wangu,
ndiyo furaha yangu; Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
(K) Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, Kuyafanya mapenzi yako.

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa.
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.
(K) Ndipo niliposema, Tazama nimekuja, Kuyafanya mapenzi yako.

Somo la 2

1Kor 1:1-3

Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu, kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu. Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.

Shangilio

Yn 12:13b

Aleluya, aleluya
Walisema, ndiye mbarikiwa
Mfalme ajaye kwa jina la Bwana,
Aleluya

Injili

Yn 1:29-34

Siku ya pili yake amwona Yesu anakuja kwake, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu, aichukuaye dhambi ya ulimwengu! Huyu ndiye niliyenena habari zake ya kwamba, Yuaja mtu nyuma yangu, ambaye amekuwa mbele yangu; kwa maana alikuwa kabla yangu. Wala mimi sikumjua; lakini kusudi adhihirishwe kwa Israeli ndiyo maana mimi nalikuja nikibatiza kwa maji. Tena Yohane akashuhudia akisema, Nimemwona Roho akishuka kama hua kutoka mbinguni; naye akakaa juu yake. Wala mimi sikumjua; lakini yeye aliyenipeleka kubatiza kwa maji, huyo aliniambia, Yeye ambaye utamwona Roho akishuka na kukaa juu yake, huyo ndiye abatizaye kwa Roho Mtakatifu. Nami nimeona, tena nimeshuhudia ya kuwa huyu ni Mwana wa Mungu.

Maoni


Ingia utoe maoni