Masomo ya Misa
Pentekoste (Jumapili, Juni 08, 2025)
Mdo 2:1-11
Hata ilipotimia siku ya Pentekoste walikuwako wote mahali pamoja. Kukaja ghafula toka mbinguni uvumi kama uvumi wa upepo wa nguvu ukienda kasi, ukaijaza nyumba yote waliyokuwa wameketi. Kukawatokea ndimi zilizogawanyikana, kama ndimi za moto uliowakalia kila mmoja wao. Wote wakajazwa Roho Mtakatifu, wakaanza kusema kwa lugha nyingine, kama Roho alivyowajalia kutamka. Na walikuwako Yerusalemu Wayahudi wakikaa, watu watauwa, watu wa kila taifa chini ya mbingu. Basi sauti hii iliposikiwa makutano walikutanika, wakashikwa na fadhaa, kwa kuwa kila mmoja aliwasikia wakisema kwa lugha yake mwenyewe. Wakashangaa wote, wakastaajabu wakiambiana, Tazama, hawa wote wasemao si Wagalilaya? Imekuwaje basi sisi kusikia kila mtu lugha yetu tuliyozaliwa nayo? Warparthi na Wamedi na Waelami, nao wakaao Mesopotamia, Uyahudi na Kapadokia, Ponto na Asia, Frigia na Pamfilia, Misri na pande za Libia karibu na Kirene, na wageni watokao Rumi, Wayahudi na waongofu, Wakrete na Waarabu; tunawasikia hawa wakisema kwa lugha zetu matendo makuu ya Mungu.
Zab 104:1, 24, 29-31, 34
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Wewe, Bwana, Mungu wangu,
Umejifanya mkuu sana;
Umejivika heshima na adhama.
Ee Bwana, jinsi yalivyo mengi matendo yako!
Kwa hekima umevifanya vyote pia.
Dunia imejaa mali zako.
(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Wewe wauficha uso wako,
Wao wanafadhaika;
Waiondoa pumzi yao, wanakufa,
Na kuyarudia mavumbi yao,
Waipeleka roho yako, wanaumbwa,
Nawe waufanya upya uso wa nchi.
(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Utukufu wa Bwana na udumu milele;
Bwana na ayafurahie matendo yake.
Kutafakari kwangu na kuwe kutamu kwake;
Mimi nitamfurahia Bwana.
(K) Waipeleka roho yako, Ee Bwana, Nawe waufanya upya uso wa nchi.
Rum 8:8-17
Wale waufuatao mwili hawawezi kumpendeza Mungu. Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake. Na Kristo akiwa ndani yenu, mwili wenu umekufa kwa sababu ya dhambi; bali roho yenu i hai, kwa sababu ya haki. Lakini, ikiwa Roho yake yeye aliyemfufua Yesu katika wafu anakaa ndani yenu, yeye aliyemfufua Kristo Yesu katika wafu ataihuisha na miili yenu iliyo katika hali ya kufa, kwa Roho wake anayekaa ndani yenu. Basi, kama ni hivyo, ndugu, tu wadeni, si wa mwili tuishi kwa kufuata mambo ya mwili, kwa maana kama tukiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa; bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi. Kwa kuwa wote wanaoongozwa na Roho wa Mungu, hao ndio wana wa Mungu. Kwa kuwa hamkupokea tena roho wa utumwa iletayo hofu; bali mlipokea roho ya kufanywa wana, ambayo kwa hiyo twalia, Aba, yaani, Baba. Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu; na kama tu watoto, basi, tu warithi; warithi wa Mungu, warithio pamoja na Kristo; naam, tukiteswa pamoja naye ili tupate na kutukuzwa pamoja naye.
Shangilio
Aleluya, aleluya
Uje Roho Mtakatifu, uzienee nyoyo za waamini wako uwatie mapendo yako.
Aleluya
Yn 14:15-16, 23-26
Siku zile Yesu aliwaambia wafuasi wake; Mkinipenda, mtazishika amri zangu. Nami nitamwomba Baba, naye atawapa Msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele; akamwambia, Mtu akinipenda, atalishika neno langu; na Baba yangu atampenda; nasi tutakuja kwake, na kufanya makao kwake. Mtu asiyenipenda, yeye hayashiki maneno yangu; nalo neno mnalolisikia silo langu, ila ni lake Baba aliyenipeleka. Hayo ndiyo niliyowaambia wakati nilipokuwa nikikaa kwenu. Lakini huyo Msaidizi, huyo Roho Mtakatifu, ambaye Baba atampeleka kwa jina langu, atawafundisha yote, na kuwakumbusha yote niliyowaambia.
Maoni
Ingia utoe maoni