Alhamisi. 21 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Sikukuu ya Kutabarukiwa Basilika la Laterani (Jumamosi, Novemba 09, 2024)  

Somo la 1

Eze 47:1-2, 8-9, 12

Malaika akanileta tena mpaka lango la nyumba; na tazama, maji yalitoka chini ya kizingiti cha nyumba, kwa njia ya mashariki, maana upande wa mbele wa nyumba ulielekea upande wa mashariki; nayo maji yakashuka toka chini ya upande wa kuume wa nyumba, upande wa kusini wa madhabahu. Ndipo akanileta nje kwa njia ya lango upande wa kaskazini, akanizungusha kwa njia ya nje mpaka lango la nje, kwa njia yake iliyoelekea mashariki; na tazama, maji yalitoka upande wa kuume. Ndipo akaniambia, Maji haya yanatoka kwenda pande za nchi ya mashariki, nayo yanashuka mpaka Araba, na kuingia katika bahari maji yatokezwayo yataingia baharini ,na maji yake yataponyeka. Tena itakuwa, kila kiumbe hai kisongamanacho, kila mahali itakapofika mito hiyo, kitaishi; kutakuwapo wingi mkubwa wa samaki, kwa sababu maji haya yamefika huko maana maji yale yataponyeka, na kila kitu kitaishi po pote utakapofikilia mto huo. Na karibu na mto, juu ya ukingo wake, upande huu na upande huu, utamea kila mti wa chakula, ambao majani yake hayatanyauka, wala matunda yake hayatatindika kamwe; utatoa matunda mapya kila mwezi, kwa sababu maji yake yanatoka mahali patakatifu; na matunda yake yatakuwa ni chakula; na majani yake yatakuwa ni dawa.

Wimbo wa Katikati

Zab 46:1-2, 4-5, 7-8

Mungu kwetu sisi ni kimbilio na nguvu,
Msaada utakaoonekana tele wakati wa mateso.
Kwa hiyo hatutaogopa ijapobadilika nchi,
Ijapotetemeka milima moyoni mwa bahari.
(K) Vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.

Kuna mto, vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu,
Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.
Mungu yu katikati yake hautatetemeshwa;
Mungu atausaidia asubuhi na mapema.
(K) Vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.

Bwana wa majeshi yu pamoja nasi,
Mungu wa Yakobo ni ngome yetu.
Njoni myatazame matendo ya Bwana,
Jinsi alivyofanya ukiwa katika nchi.
(K) Vijito vyake vyaufurahisha mji wa Mungu, Patakatifu pa maskani zake Aliye juu.

Somo la 2

1Kor 3:9-11, 16-17

Ninyi ni jingo la Mungu. Kwa kadiri ya neema ya Mungu niliyopewa, mimi, kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake. Lakini kila mtu na aangalie jinsi anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani, yesu Kristo. Lakini kama mtu akijenga juu ya msingi huo, dhahabu au fedha au mawe ya thamani, au miti au majani, au manyasi, kazi ya kila mtu itakuwa Dhahiri. Maana siku ile itaidhihirisha, kwa kuwa yafunuliwa katika moto; na ule moto wenyewe utaijaribu kazi ya kila mtu, ni ya namna gani. Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, nay a kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu? Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

Shangilio

2Nya 7:16

Aleluya, aleluya,
Nimeichagua nyumba hii na kuitakasa, asema Bwana, ili kwamba jina langu lipate kuwako huko milele.
Aleluya.

Injili

Yn 2:13-22

Pasaka ya Wayahudi ilikuwa karibu; naye Yesu alikwea mpaka Yerusalemu. Akaona pale hekaluni watu waliokuwa wakiuza ng’ombe na kondoo na njiwa, na wenye kuvunja fedha wameketi. Akafanya kikoto cha kambaa, akawatoa wote katika hekalu, na kondoo na ng’ombe; akamwaga fedha za wenye kuvunja fedha, akazipindua meza zao; akawaambia wale waliokuwa wakiuza njiwa, Yaondoeni haya; msiifanye nyumba ya Baba yangu kuwa nyumba ya biashara. Wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa imeandikwa, Wivu wa nyumba yako utanila. Basi Wayahudi wakajibu, wakamwambia, Ni ishara gani utuonyeshayo, kwamba unafanya haya? Yesu akajibu, akawaambia, Livunjeni hekalu hili, name katika siku t atu nitalisimamisha. Basi Wayahudi wakasema, Hekalu hili lilijengwa katika muda wa miaka arobaini na sita, nawe utalisimamisha katika siku tatu? Lakini yeye alinena habari za hekalu la mwili wake. Basi alipofufuka katika wafu, wanafunzi wake wakakumbuka ya kuwa alisema hivi, wakaliamini lile andiko na lile neno alilolinena Yesu.

Maoni

Alfredy Kilala

Tumshukuru Mungu

Ingia utoe maoni