Jumanne. 22 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 29 ya Mwaka (Jumapili, Oktoba 20, 2024)  

Somo la 1

Isa. 53:10-11

Bwana aliridhika kumchubua; Amemhuzunisha; Utakapofanya nafsi yake kuwa dhabihu kwa dhambi, Ataona uzao wake, ataishi siku nyingi; Na mapenzi ya Bwana yatafanikiwa mkononi mwake; Ataona mazao ya taabu ya nafsi yake, na kuridhika. Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwenye haki atawafanya wengi kuwa wenye haki; Naye atayachukua maovu yao.

Wimbo wa Katikati

Zab. 33:4-5, 18-20,22

Neno la Bwana lina adili,
Na kazi yake yote huitenda kwa uaminifu.
Huzipenda haki na hukumu,
Nchi imejaa fadhili za Bwana.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Tazama, jicho la Bwana li kwao wamchao,
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti,
Na kuwahuisha wakati wa njaa.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Nafsi zetu ninamngoja Bwana,
Yeye ndiye msaada wetu na ngao yetu.
Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi,
Kama vile tunavyokungoja Wewe.
(K) Ee Bwana, fadhili zako zikae nasi, kama vile tulivyokungoja Wewe.

Somo la 2

Ebra. 4:14-16

Iwapo tunaye kuhani mkuu aliyeingia katika mbingu, Yesu, Mwana wa Mungu, na tuyashike sana maungano yetu. Kwa kuwa hatuna kuhani mkuu asiyeweza kuchukuana nasi katika mambo yetu ya udhaifu; bali yeye alijaribiwa sawasawa na sisi katika mambo yote, bila kufanya dhambi. Basi na tukikaribie kiti cha neema kwa ujasiri, ili tupewe rehema, na kupata neema ya kutusaidia wakati wa mahitaji.

Shangilio

Efe. 1:17,18

Aleluya, aleluya!
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Uyatie nuru macho ya mioyo yetu, ili tujue tumaini la mwito wake jinsi lilivyo.
Aleluya.

Injili

Mk. 10:35-45

Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo, walimwendea, wakamwambia, Mwalimu, twataka utufanyie lolote tutakalokuomba. Akawaambia, Mwataka niwafanyie nini? Wakamwambia, Utujalie sisi tuketi, mmoja mkono wako wa kushoto, katika utukufu wako. Yesu akawaambia, Hamjui mnaloliomba. Mwaweza kunywea kikombe ninyweacho mimi, au kubatizwa ubatizo nibatizwao mimi? Wakamwambia, Twaweza. Yesu akawaambia, Kikombe ninyweacho mimi mtakinywea, na ubatizo nibatizwao mimi mtabatizwa; lakini habari ya kuketi mkono wangu wa kuume au mkono wangu wa kushoto si langu kuwapa, ila wao watapewa waliowekewa tayari. Hata wale kumi waliposikia wakaanza kuwakasirikia Yakobo na Yohane. Yesu akawaita, akawaambia, Mwajua ya kuwa wale wanaohesabiwa kuwa wakuu wa Mataifa huwatawala kwa nguvu, na wakubwa wao huwatumikisha. Lakini haitakuwa hivyo kwenu; bali mtu anayetaka kuwa mkubwa kwenu, atakuwa mtumishi wenu, na mtu anayetaka kuwa wa kwanza wenu, atakuwa mtumwa wa wote. Kwa maana Mwana wa Adamu naye hakuja kutumikiwa, bali kutumika, na kutoa nafsi yake iwe fidia ya wengi.

Maoni


Ingia utoe maoni