Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 2 ya Majilio (Jumatano, Desemba 07, 2016)  

Somo la 1

Isa 40:25-31

Mtanifananisha na nani, basi, nipate kuwa sawa naye? Asema yeye aliye Mtakatifu. Inueni macho yenu juu, mkaone; ni nani aliyeziumba hizi; aletaye nje jeshi lao kwa hesabu; aziita zote kwa majina; kwa ukuu wa uweza wake, na kwa kuwa yeye ni hodari kwa nguvu zake; hapana moja isiyokuwapo mahali pake. Mbona unasema, Ee Yakobo, mbona unanena, Ee Israeli, Njia yangu imefichwa, Bwana asiione, na hukumu yangu imempita Mungu wangu asiiangalie? Je! Wewe hukujua? Hukusikia? Yeye Mungu wa milele, Bwana, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki. Huwapa nguvu wazimiao, humwongezea nguvu yeye asiyekuwa na uwezo. Hata vijana watazimia na kuchoka, na wanaume vijana wataanguka; bali wao wamngojeao Bwana watapata nguvu mpya; watapanda juu kwa mbawa kama tai; watapiga mbio, wala hawatachoka; watakwenda kwa miguu, wala hawatazimia.

Wimbo wa Katikati

Zab 103:1-4, 8, 10

Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K)Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema,
(K)Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Hakututenda sawasawa na hatia zetu,
Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu.
(K)Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Tazama Bwana atakuja kuwaokoa watu wake, Heri walio tayari kumlaki.
Aleluya.

Injili

Mt 10:28-30

Yesu aliwaambia makutano: Msiwaogope wauuao mwili, wasiweze kuiua na roho; afadhali mwogopeni yule awezaye kuangamiza mwili na roho pia katika jehanum. Je! Mashomoro wawili hawauzwi kwa senti moja? Wala hata mmoja haanguki chini asipojua Baba yenu; lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote.

Maoni


Ingia utoe maoni