Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 10 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 14, 2024)  

Somo la 1

1 Fal 19:9a, 11-16

Eliya alifika kunako pango, akalala ndani yake. Akasema, Toka, usimame mlimani mbele za Bwana. Na tazama, Bwana akapita; upepo mwingi wa nguvu ukaipasua milima, ukaivunja-vunja miamba mbele za Bwana; lakini Bwana hakuwamo katika upepo ule; na baada ya upepo, tetemeko la nchi; lakini Bwana hakuwamo katika lile tetemeko la nchi; na baada ya tetemeko la nchi kukawa na moto; lakini Bwana hakuwamo katika moto ule; na baada ya moto sauti ndogo, ya utulivu. Ikawa, Eliya alipoisikia, alijifunika uso wake katika mavazi yake, akatoka, akasimama mlangoni mwa pango. Na tazama, sauti ikamjia, kusema, Unafanya nini hapa, Eliya? Akasema, Nimeona wivu mwingi kwa ajili ya Bwana, Mungu wa majeshi; kwa kuwa wana wa Israeli wameyaacha maagano yako, na kuzivunja madhabahu zako, na kuwaua manabii wako kwa upanga; nami nimesalia, mimi peke yangu; nao wanitafuta roho yangu waiondoe. Bwana akamwambia, Enenda, urudi njia ya jangwa la Dameski; ukifika, mtie mafuta Hazaeli awe mfalme wa Shamu. Na Yehu mwana wa Nimshi mtie mafuta awe mfalme wa Israeli; na Elisha mwana wa Shafati wa Abel-Mehola mtie mafuta awe nabii mahali pako.

Wimbo wa Katikati

Zab 27:7-9, 13-14

Ee Bwana, usikie, kwa sauti yangu ninalia, Unifadhili, unijibu.
Uliposema, Nitafuteni uso wangu, Moyo wangu umekuambia,
(K)Usinifiche uso wako, Ee Bwana

Bwana, uso wako nitautafuta.
Usinifiche uso wako, Usijiepushe na mtumishi wako kwa hasira.
Umekuwa msaada wangu, usinitupe, Wala usiniache, Ee Mungu wa wokovu wangu.
(K)Usinifiche uso wako, Ee Bwana

Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana Katika nchi ya walio hai.
Umngoje Bwana, uwe hodari, Upige moyo konde, naam, umngoje Bwana.
(K)Usinifiche uso wako, Ee Bwana

Shangilio

Fil 2:15d, 16a

Aleluya, aleluya
Mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu, mkishika neno la uzima.
Aleluya

Injili

Mt 5:27-32

Yesu aliwaambia wanafunzi: Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake. Jicho lako la kuume likikukosesha, ling'oe ulitupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Na mkono wako wa kuume ukikukosesha, ukate uutupe mbali nawe; kwa maana yakufaa kiungo chako kimoja kipotee wala mwili wako mzima usitupwe katika jehanum. Imenenwa pia, Mtu akimwacha mkewe, na ampe hati ya talaka; lakini mimi nawaambia, Kila mtu amwachaye mkewe, isipokuwa kwa habari ya uasherati, amfanya kuwa mzinzi; na mtu akimwoa yule aliyeachwa, azini.

Maoni


Ingia utoe maoni