Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Bikira Maria Kwenda Kumwamkia Elizabeti (Ijumaa, Mei 31, 2024)  

Somo la 1

Sef 3:14-18

Imba, Ee binti Sayuni; piga kelele, Ee Israeli; Furahi na kushangilia kwa moyo wako wote, Ee binti Yerusalemu. Bwana ameziondoa hukumu zako, Amemtupa nje adui yako; Mfalme wa Israeli, naam, yeye Bwana, yu katikati yako; Hutaogopa uovu tena. Katika siku ile Yerusalemu utaambiwa, Usiogope, Ee Sayuni; mikono yako isilegee. Bwana, Mungu wako, yu katikati yako shujaa awezaye kuokoa; Atakushangilia kwa furaha kuu, Atakutuliza katika upendo wake, Atakufurahia kwa kuimba. Nitawakusanya wanaousikitikia mkutano wa ibada, hao waliokuwa wa kwako; ambao mzigo uliokuwa juu yake ulikuwa fedheha kwao.

Wimbo wa Katikati

Isa 12:2-6

Tazama, Mungu ndiye wokovu wangu;
Nitatumaini wala sitaogopa;
Maana Bwana Yeshova ni nguvu zangu na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Basi, kwa furaha mtateka maji katika visima vya wokovu.
(K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

Mshukuruni Bwana, liitieni jina lake;
Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa,
Litajeni jina lake kuwa limetukuka.
(K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.


Mwimbieni Bwana; kwa kuwa ametenda makuu;
Na yajulikane haya katika dunia yote.
Paza sauti, piga kelele, mwenyeji wa Sayuni;
Maana Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.
(K) Mtakatifu wa Israeli ni mkuu kati yako.

Shangilio

Lk 1:45

Aleluya.
Heri Bikira Maria aliyesadiki ya kuwa aliyoambiwa na Bwana yatatimizwa.
Aleluya.

Injili

Lk 1:39-56

Mariamu aliondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda, akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia, Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Mariamu, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa. Limenitokeaje neno hili, hata mama wa Bwana wangu anijilie mimi? Maana sauti ya kuamkia kwako ilipoingia masikioni mwangu, kitoto kichanga kikaruka kwa shangwe ndani ya tumbo langu. Naye heri aliyesadiki; kwa maana yatatimizwa aliyoambiwa na Bwana. Mariamu akasema, Moyo wangu wamwadhimisha Bwana, Na roho yangu imemfurahia Mungu, Mwokozi wangu; kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake. Kwa maana, tazama, tokea sasa vizazi vyote wataniita mbarikiwa; Kwa kuwa mwenye nguvu amenitendea makuu, na jina lake ni takatifu. Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi kwa hao wanaomcha. Amefanya nguvu kwa mkono wake; Amewatawanya walio na kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewaangusha wakuu katika ivti vyao vya enzi; na wanyonge amewakweza. Wenye njaa amewashibisha mema, Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu. Amemsaidia Israeli, mtumishi wake; Ili kukumbuka rehema zake; Kama alivyowaambia baba zetu, Ibrahimu na uzao wake hata milele. Mariamu akakaa naye kadiri ya miezi mitatu, kisha akarudi kwenda nyumbani kwake.

Maoni


Ingia utoe maoni