Jumanne. 07 Mei. 2024

Masomo ya Misa

Sherehe ya Kupashwa Habari Bikira Maria ya kuzaliwa kwa Bwana (Jumatatu, Aprili 08, 2024)  

Somo la 1

Isa 7:10–14

Bwana alisema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sana, enyi nyumba ya Daudi; Je! Ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

Wimbo wa Katikati

Zab 40:6–10

Dhabihu na matoleo hukupendezwa nazo,
Masikio yangu umeyazibua,
Kafara na sadaka za dhambi hukuzitaka.
Ndipo niliposema, Tazama nimekuja.
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Katika gombo la chuo nimeandikiwa
Kuyafanya mapenzi yako,
Ee Mungu wangu, ndiyo furaha yangu;
Naam, sheria yako imo moyoni mwangu.
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Nimehubiri habari za haki katika kusanyiko kubwa,
Sikuizuia midomo yangu; Ee Bwana, unajua.
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Sikusitiri haki yako moyoni mwangu;
Nimetangaza uaminifu wako na wokovu wako.
Sikuficha fadhili zako wala kweli yako
Katika kusanyiko kubwa.
(K) Tazama, nimekuja, Ee Bwana, kuyafanya mapenzi yako.

Somo la 2

Ebr 10:4–10

Haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi. Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari; Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo; Ndipo niliposema, Tazama nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) niyafanye mapenzi yako, Mungu. Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati), ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili. Katika mapenzi hayo tumepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

Shangilio

Yn 1:14

Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu, nasi tukaona utukufu wake.

Injili

Lk 1:26-38

Mwezi wa sita, malaika Gabrieli alitumwa na Mungu kwenda mpaka mji wa Galilaya, jina lake Nazareti, kwa mwanamwali bikira aliyekuwa ameposwa na mtu, jina lake Yusufu, wa mbari ya Daudi; na jina lake bikira huyo ni Mariamu. Akaingia nyumbani kwake akasema, Salamu, uliyepewa neema. Bwana yu pamoja nawe. Naye akafadhaika sana kwa ajili ya maneno yake, akawaza moyoni, Salamu hii ni ya namna gani? Malaika akamwambia, Usiogope, Mariamu, kwa maana umepata neema kwa Mungu. Tazama, utachukua mimba na kuzaa mtoto mwanamume; na jina lake utamwita Yesu. Huyo atakuwa mkuu, ataitwa Mwana wa Aliye ju, na Bwana Mungu atampa kiti cha enzi cha Daudi, baba yake. Ataimiliki nyumba ya Yakobo hata milele, na ufalme wake utakuwa hauna mwisho. Mariamu akamwambia malaika, Litakuwaje neno hili, maana sijui mume? Malaika akajibu akamwambia, Roho Mtakatifu atakujilia juu yako, na nguvu zake Aliye juu zitakufunika kama kivuli; kwa sababu hiyo hicho kitakachozaliwa kitaitwa kitakatifu, Mwana wa Mungu. Tena, tazama, jamaa yako Elisabeti naye amechukua mimba ya mtoto mwanamume katika uzee wake; na mwezi huu ni wa sita kwake yeye aliyeitwa tasa; kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu. Mariamu akasema, Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; na iwe kwangu kama ulivyosema. Kisha malaika akaondoka akaenda zake.

Maoni

Martin Muteti

Amina

Ingia utoe maoni