Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 32 ya Mwaka (Ijumaa, Novemba 11, 2016)  

Somo la 1

2 Yn 1:4-9

Nalifurahi mno kwa kuwa nimewaona baadhi ya watoto wako wanaenenda katika kweli, kama vile tulivyopokea amri kwa Baba. Na sasa mama, nakuomba, si kwamba nakuandikia amri mpya, bali ile tuliyokuwa nayo tangu mwanzo, kwamba tupendane. Na huu ndio upendo: tuenende kwa kuzifuata amri zake. Hii ndiyo ile amri, kama mlivyosikia tangu mwanzo kwamba mwenende katika hiyo. Kwa maana wadanganyifu wengi wametokea duniani, wasiokiri ya kuwa Yesu Kristo yuaja katika mwili. Huyo ndiye yule mdanganyifu na mpinga Kristo. Jiangalieni nafsi zenu msiyapoteze mliyoyatenda, bali mpokee thawabu timilifu. Kila apitaye cheo, wala asidumu katika mafundisho ya Kristo, yeye hana Mungu. Yeye adumuye katika mafundisho hayo, huyo ana Baba na Mwana pia.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:1-2, 10-11, 17-18

Heri walio kamili njia zao,
Waendao katika sheria ya Bwana.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Heri wazitiio shuhuda zake,
Wamtafutao kwa moyo wote.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Kwa moyo wangu wote nimekutafuta,
Usiniache nipotee mbali na maagizo yako.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Moyoni mwangu nimeliweka neno lako,
Nisije nikakutenda dhambi.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Umtendee mtumishi wako ukarimu,
Nipate kuishi, nami nitalitii neno lako.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Unifumbue macho yangu niyatazame Maajabu yatokayo katika sheria yako.
(K) Heri waendao katika sheria ya Bwana.

Shangilio

Zab. 119:28, 33

Aleluya, aleluya,
Unitie nguvu sawasawa na neno lako, Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya.

Injili

Lk 17:26-37

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Na kama ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku zake Mwana wa Adamu. Walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakioa na kuolewa, hata siku ile Nuhu aliyoingia katika safina, gharika ikashuka ikawaangamiza wote. Na kadhalika, kama ilivyokuwa katika siku za Lutu, walikuwa wakila na kunywa, walikuwa wakinunua na kuuza, wakipanda na kujenga; lakini siku ile Lutu aliyotoka Sodoma kulinyesha moto na kibiriti kutoka mbinguni vikawaangamiza wote. Hivyo ndivyo itakavyokuwa siku ile atakayofunuliwa Mwana wa Adamu. Katika siku ile, aliye juu ya dari, na vyombo vyake vimo ndani ya nyumba, asishuke ili kuvitwaa; na kadhalika, aliye shambani asirejee nyuma. Mkumbukeni mkewe Lutu. Mtu ye yote atakaye kuiponya nafsi yake, ataiangamiza; na ye yote atakayeiangamiza ataiponya. Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa. Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.] Wakajibu, wakamwuliza, Wapi, Bwana? Akawaambia, Ulipo mzoga, ndipo watakapokutanika tai.

Maoni


Ingia utoe maoni