Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Alhamisi ya Kipindi cha Noeli (Alhamisi, Januari 04, 2024)  

Somo la 1

1Yoh 3:7-10

Watoto wadogo, mtu na asiwadanganye; atendaye haki yu na haki kama yeye alivyo na haki; atendaye dhambi ni wa Ibilisi; kwa kuwa Ibilisi hutenda dhambi tangu mwanzo. Kwa kusudi hili Mwana wa Mungu alidhihirishwa, ili azivunje kazi za Ibilisi. Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu. Katika hili watoto wa Mungu ni dhahiri, na watoto wa Ibilisi nao. Mtu yeyote asiyetenda haki hatokani na Mungu, wala yeye asiyempenda ndugu yake.

Wimbo wa Katikati

Zab 98:1, 7-9

Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe pamoja kwa furaha,
Mbele za Bwana,
Kwa maana anakuja aihukumu nchi.
(K) Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili.
(K) Miisho yote ya dunia, imeuona Wokovu wa Mungu wetu.

Shangilio

Ebr 1:1-2

Aleluya, aleluya,
Baada ya Mungu kusema zamani mara nyingi, na kwa namna nyingi na baba zetu kwa kinywa cha manabii, Siku hizi zilizo za mwisho amesema nasi kwa kinywa cha Mwana.
Aleluya.

Injili

Yn 1:35-42

Siku ile, Yohana alikuwa amesimama pamoja na wawili katika wanafunzi wake. Akamtazama Yesu akitembea, akasema, Tazama, Mwana-kondoo wa Mungu! Wale wanafunzi wawili wakamsikia akinena, wakamfuata Yesu. Yesu aligeuka, akawaona wakimfuata, akawaambia, Mnatafuta nini? Wakamwambia, Rabi, (maana yake, Mwalimu), unakaa wapi? Akawaambia, Njoni, nanyi mtaona. Wakaenda, wakaona akaapo, wakakaa kwake siku ile. Nayo ilikuwa yapata saa kumi. Andrea, nduguye Simoni Petro, alikuwa mmoja wa wale wawili waliomsikia Yohane na kumfuata Yesu. Huyo akamwona kwanza Simoni, ndugu yake mwenyewe, akamwambia, Tumemwona Masihi (maana yake, Kristo). Akampeleka kwa Yesu. Naye Yesu akamtazama, akasema, Wewe u Simoni, mwana wa Yohane; nawe utaitwa Kefa (tafsiri yake Petro, au Jiwe).

Maoni


Ingia utoe maoni