Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 3 ya Majilio (Jumapili, Desemba 17, 2023)  

Somo la 1

Isa 61:1-2, 10-11

Roho ya Bwana Mungu I juu yangu; kwa sababu Bwana amenitia mafuta, niwahubiri wanyenyekevu habari njema; amenituma ili kuwaganga waliovunjika moyo, kuwatangazia mateka uhuru wao, na hao waliofungwa habari za kufungukiwa kwao. Kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa, na siku ya kisasi cha Mungu wetu. Nitafurahi sana katika Bwana, nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu; maana amenivika mavazi ya wokovu, amenifunika vazi la haki, kama bwana arusi ajipambavyo kwa kilemba cha maua,na kama bibi arusi ajipambavyo kwa vyombo vya dhahabu. Maana kama nchi itoavyo machipuko yake, na kama bustani ioteshavyo vitu vilivyopandwa ndani yake; ndivyo Bwana Mungu atakavyootesha haki na sifa mbele ya mataifa yote.<

Wimbo wa Katikati

Lk 1:46-50

Moyo wangu wamwadhimisha Bwana,
Na roho yangu imemfurahi Mungu, Mwokozi wangu;
Kwa kuwa ameutazama unyonge wa mjakazi wake.
Kwa maana, tazama, toka sasa
Vizazi vyote wataniita mbarikiwa;
(K) Nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu.

Kwa kuwa Mwenye nguvu amenitendea makuu,
Na jina lake ni takatifu.
Na rehema zake hudumu vizazi hata vizazi
Kwa hao wanaomcha.
(K) Nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu.

Wenye njaa amewashibisha mema,
Na wenye mali amewaondoa mikono mitupu.
Amemsaidia Israeli, mtumishi wake;
Ili kukumbuka rehema zake.
(K) Nafsi yangu itashangilia katika Mungu wangu.

Somo la 2

1Thes 5:16-24

Furahini siku zote; ombeni bila kukoma; shukuruni kwa kila jambo; maana hayo ni mapenzi ya Mungu kwenu katika Kristo Yesu. Msimzimishe Roho; msitweze unabii; jaribuni mambo yote; lishikeni lililo jema; jitengeni na ubaya wa kila namna. Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi nafsi zenu na roho zenu na miili yenu mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye ni mwaminifu ambaye awaita, naye atafanya.

Shangilio

Lk 4:18

Aleluya,aleluya
Roho wa Bwana yu juu yangu, Amenituma kuwahubiri maskini habari njema;
Aleluya

Injili

Yh 1:6-8, 19-28

Palitokea mtu, ametumwa kutoka kwa Mungu, jina lake Yohane. Huyo alikuja kwa ushuhuda, ili aishuhudie ile nuru, wote wapate kuamini kwa yeye. Huyo hakuwa ile nuru, bali alikuja ili aishuhudie ile nuru. Na huu ndio ushuhuda wake Yohane, Wayahudi walipotuma kwake makuhani na Walawi kutoka Yerusalemuili wamwulize, Wewe u nani? Naye alikiri, wala hakukana; alikiri kwamba, Mimi siye Kristo. Wakamwuliza, Ni nani basi? U Eliya wewe? Akasema, Mimi siye. Wewe u nabii yule? Akajibu, La. Basi wakamwambia, U nani? Tuwape majibu wale waliotupeleka. Wanenaje juu ya nafsi yako? Akasema, Mimi ni sauti ya mtu aliaye nyikani, Inyosheni njia ya Bwana kama vile alivyonena nabii Isaya. Nao wale waliotumwa walikuwa wametoka kwa Mafarisayo. Wakamwuliza, wakamwambia, Mbona basi wabatiza, ikiwa wewe si Kristo, wala Eliya, wala nabii yule? Yohane akawajibu akisema, Mimi nabatiza kwa maji. Katikati yenu amesimama yeye msiyemjua ninyi. Ndiye yule ajaye nyuma yangu, ambaye mimi sistahili kuilegeza gidamu ya kiatu chake. Hayo yalifanyika huko Bethania ng'ambo ya Yordani, alikokuwako Yohane akibatiza.

Maoni


Ingia utoe maoni