Jumatano. 30 Oktoba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 32 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 06, 2016)  

Somo la 1

2 Mak. 7:1-2, 9-14

Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Mmoja akajifanya mnenaji wao akasema, Wataka kuuliza nini na kujua nini juu yetu? Sisi tu tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu. Wa pili alipokuwa kufani alisema, Wewe mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele. Na baada yake alidhihakiwa yule wa tatu. Naye mara alipoagizwa, alitoa ulimi wake, akanyosha mikono yake bila hofu, akasema kwa ushujaa, Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena. Hata mfalme na watu wake walishangazwa kwa roho ya kijana huyu, kwa jinsi alivyodharau maumivu yake. Akiisha kufa huyu walimtesa na wa nne na kumtendea mabaya yale yale. Naye alipokaribia kufa alisema hivi; Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo.

Wimbo wa Katikati

Zab 17:1, 5-6, 8, 15

Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.
(K) Ee Bwana niamkapo nitashibishwa kwa sura yako.

Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu.
(K) Ee Bwana niamkapo nitashibishwa kwa sura yako.

Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
(K) Ee Bwana niamkapo nitashibishwa kwa sura yako.

Bali mimi nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako.
(K) Ee Bwana niamkapo nitashibishwa kwa sura yako.

Somo la 2

2 The 2:16-3:1-5

Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.

Shangilio

Yn 1:12,14

Aleluya, aleluya
Naye neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya

Injili

Lk 20:27-38

Baadhi ya Masadukayo wakamwendea, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili [akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto;] hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi; wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.

Maoni


Ingia utoe maoni