Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 1 ya Majilio (Jumapili, Desemba 03, 2023)  

Somo la 1

Isa 63:16-17; 64:1, 4-8

Wewe, Bwana, ndiwe Baba yetu, mkombozi wetu tangu milele ndilo jina lako. Ee Bwana, mbona umetukosesha njia zako, ukatufanyiza kuwa na mioyo migumu hata tusikuogope? Urudi kwa ajili ya watumishi wako, kabila za urithi wako. Laiti ungepasua mbingu, na kushuka, ili milima iteleme mbele zako. Maana tangu zamani za kale watu hawakusikia, wala kufahamu kwa masikio, wala jicho halikuona Mungu, ila wewe, atendaye mambo kwa ajili yake amngojaye.

Wwe wamlaki yeye afurahiaye yaliyo haki na kuyatenda, watu wale wakukumbukao katika njia zako; tazama, ulikuwa na hasira, nasi tulitenda dhambi; tumekuwa katika mambo haya muda mwingi; nasi, je! Tukaokolewa? Kwa maana sisi sote tumekuwa kama mtu aliye mchafu, na matendo yetu yote ya haki yamekuwa kama nguo iliyotiwa unajisi; sisi sote twanyauka kama jani, na maovu yetu yatuondoa, kama upepo uondoavyo. Tena hapana aliitiaye jina lako, ajitahidiye akushike; kwa kuwa umetuficha uso wako, nawe umetukomesha kwa njia ya maovu yetu. Lakini sasa, Ee Bwana, wewe u baba yetu; sisi tu udongo, nawe u mfinyanzi wetu; sisi sote tu kazi ya mikono yako.

Wimbo wa Katikati

Zab 80:1-2, 14-15, 17-18

Wewe uchungaye Israeli usikie,
Wewe uketiye juu ya makerubi, utoe nuru.
Uziamshe nguvu zako.
Uje, utuokoe.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Ee Mungu wa majeshi, tunakusihi, urudi,
Utazame toka juu uone, uujilie mzabibu huu.
Na mche ule ulioupanda
Kwa mkono wako wa kuume;
Na tawi lile ulilolifanya
Kuwa imara kwa nafsi yako.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Mkono wako na uwe juu yake
Mtu wa mkono wako wa kuume;
Juu ya mwanadamu uliyemfanya
Kuwa imara kwa nafsi yako;
Basi hatutakuacha kwa kurudi nyuma;
Utuhuishe nasi tutaliitia jina lako.
(K) Ee Mungu, uturudishe, uangazishe uso wako nasi tutaokoka.

Somo la 2

1Kor 1:3-9

Ndugu zangu, neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo. Namshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kwa sababu ya neema ya Mungu mliyopewa katika Kristo Yesu; kwa kuwa katika kila jambo mlitajirika katika yeye, katika maneno yote, na maarifa yote; kama ushuda wa Kristo ulivyothibita kwenu; hata hamkupungukiwa na karama yoyote, mkikutazamaia sana kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambaye atawathitisha hata mwisho, ili msilaumiwe siku ile ya Bwana wetu Yesu Kristo. Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa nay eye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu.

Shangilio

Zab 85:7

Aleluya, Aleluya,
Ee Bwana utuonyeshe rehema zako utupe wokovu wako,
Aleluya.

Injili

Mk 13:33-37

Siku ile: Yesu aliwaambia wafuasi wake: Angalieni, kesheni, (ombeni), kwa kuwa hamjui wakati ule utakapokuwapo. Mfano wake ni kama mtu mwenye kusafiri, ameicha nyumba yake, amewapa watumwa wake amri, na kila mtu kazi yake, naye amemwamuru bawabu akeshe. Kesheni basi, kwa maana hamjui ajapo bwana wa nyumba, kwamba ni jioni, au kwamba ni usiku wa manane, au awikapo jimbi, au asubuhi; asije akawasili ghafula akawakuta mmelala. Na hilo niwaambialo ninyi, nawaambia wote, Kesheni.

Maoni


Ingia utoe maoni