Masomo ya Misa
Dominika ya 31 ya Mwaka (Jumapili, Novemba 05, 2023)
Mal 1:14-2:2, 8-10
Kwa maana mimi ni Mfalme mkuu, asema Bwana wa majeshi, na jina langu latisha katika Mataifa.Na sasa, enyi makuhani, amri hii yawahusu ninyi. Kama hamtaki kusikia, na kama hamtaki kuitia moyoni, ili kulitukuza jina langu, asema Bwana wa majeshi, basi nitawapelekeeni laana, nami nitazilaani baraka zenu; Bali ninyi mmegeuka mkaiacha njia; mmewakwaza watu wengi katika sheria; mmeliharibu agano la Lawi, asema Bwana wa majeshi. Kwa sababu hiyo mimi nami nimewafanya ninyi kuwa kitu cha kudharauliwa, na unyonge, mbele ya watu wote, kama vile ninyi msivyozishika njia zangu, bali mmewapendelea watu katika sheria. Je! Sisi sote hatuna Baba mmoja? Mungu aliyetuumba siye mmoja tu? Basi, mbona kila mmoja wetu anamtenda ndugu yake mambo ya hiana, tukilinajisi agano la baba zetu?
Zab 131
Bwana, moyo wangu hauna kiburi,
Wala macho yangu hayainuki.
Wala sijishughulishi na mambo makuu,
Wala na mambo yashindayo nguvu zangu.
(K) Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako.
Hakika nimeituliza nafsi yangu,
Na kuinyamazisha.
Kama mtoto aliyeachishwa Kifuani mwa mama yake;
Kama mtoto aliyeachishwa,
Ndivyo roho yangu ilivyo kwangu.
(K) Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako.
Ee Israeli, umtarajie Bwana,
Tangu leo na hata milele.
(K) Ee Bwana, uilinde nafsi yangu katika amani yako.
1Thes 2:7-9,13
Kama vile mlezi awatunzavyo watoto wake mwenyewe. Vivyo hivyo nasi tukiwatumaini kwa upendo mwingi, tuliona furaha kuwapa, si Injili ya Mungu tu, bali na roho zetu pia, kwa sababu mmekuwa wapendwa wetu. Maana, ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi pia ndani yenu ninyi mnaoamini.
Yn 6:63, 68
Aleluya, aleluya
Bwana maneno yako ni roho tena ni uzima, wewe unayo maneno ya uzima wa milele,
Aleluya
Mt 23:1-12
Yesu aliwaambia makutano na wanafunzi wake, akasema, Waandishi na Mafarisayo wameketi katika kiti cha Musa; basi, yo yote watakayowaambia, myashike na kuyatenda; lakini kwa mfano wa matendo yao, msitende; maana wao hunena lakini hawatendi. Wao hufunga mizigo mizito na kuwatwika watu mabegani mwao; wasitake wenyewe kuigusa kwa kidole chao. Tena matendo yao yote huyatenda ili kutazamwa na watu; kwa kuwa hupanua hirizi zao, huongeza matamvua yao; hupenda viti vya mbele katika karamu, na kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni, na kuitwa na watu, Rabi. Bali ninyi msiitwe Rabi, maana mwalimu wenu ni mmoja, nanyi nyote ni ndugu. Wala msimwite mtu baba duniani; maana Baba yenu ni mmoja, aliye wa mbinguni. Wala msiitwe viongozi; maana kiongozi wenu ni mmoja, naye ndiye Kristo. Naye aliye mkubwa wenu atakuwa mtumishi wenu. Na ye yote atakayejikweza, atadhiliwa; na ye yote atakayejidhili, atakwezwa.
Maoni
jonas julius john
asante sanaIngia utoe maoni