Jumamosi. 23 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 25 ya Mwaka (Jumatano, Septemba 27, 2023)  

Somo la 1

Ezr 9:5-9

Wakati wa sadaka ya jioni, mimi Ezra niliinuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu wangu; nikasema, Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga, tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika kufungwa kwetu. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, tuisimamishe nyumba ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.

Wimbo wa Katikati

Tob 13:2-4, 6

Kwa maana hurudi, na kurehemu tena;
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Enyi bani Israeli, mshukuruni mbele ya mataifa
Yeye ambaye ametutawanya katikati yao.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Kuko huko utangazeni ukuu wake,
Mwadhimisheni mbele ya wote walio hai;
Kwa kuwa Yeye ndiye Bwana wetu,
Naye Mungu yu Baba wetu,
Naye Mungu yu Baba yetu milele.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.

Shangilio

Shangilio

Aleluya, aleluya,
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana. Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya.

Injili

Lk 9:1-6

Yesu aliwaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi. Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate, wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na nyumba yoyote mtakayoingia kaeni humo, tokeni humo. Na wale wasiowakaribisha, mtokakpo katika mji huo yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. Wakaenda, wakazunguka katika vijiji, wakihubiri Injili, na kupoza watu kila mahali.

Maoni


Ingia utoe maoni