Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatatu ya 14 ya Mwaka (Jumatatu, Julai 10, 2023)  

Somo la 1

Mwa. 28:10-22

Yakobo alitoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulanl akakaa huko usiku kucha, maana jua lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamisha juu ya nchi, na ncha yake yafika mbinguni. Tena, tazama. malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, Bwana amesimama juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka katika usingizi wake, akasema, Kweli, Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli; lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililosimamisha kama nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.

Wimbo wa Katikati

Zab 91:1-4, 14-15

Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
Na katika tauni iharibuyo.
Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;
Uaminifu wake ni ngao na kigao.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nilamwitikia;
NitaKuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.

Shangilio

Lk.8:15

Aleluya, aleluya,
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao, hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya.

Injili

Mt 9:18-26

Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata, pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake, Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu, binti yangu, imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.

Maoni


Ingia utoe maoni