Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 5 ya Pasaka (Jumanne, Mei 09, 2023)  

Somo la 1

Mdo 14:19-28

Wayahudi walifika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa. Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe. Hata walipokwisha kuhubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia, wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi. Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawa weka katika mikono ya Bwana waliyemwamini. Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia. Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia. Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza. Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, waka- waeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani. Wakaketi huko wakati usiokuwa mcha che, pamoja na wanafunzi.

Wimbo wa Katikati

Zab 145:10-13, 21

Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako,
Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
(K) Watawajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari wa zamani zote.

Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
(K) Watawajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari wa zamani zote.

Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
Wote wenye mwili na walihimidi jina lake
takatifu milele na milele.
(K) Watawajulisha watu matendo yake makuu, Na utukufu wa fahari wa zamani zote.

Shangilio

Ufu 1:5

Aleluya, aleluya,
Ee Kristo, yu shahidi aliye mwaminifu, mzaliwa wa kwanza wa waliokufa, na mkuu wa wafalme wa dunia.
Aleluya.

Injili

Yn 14:27-31

Siku ile, Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Amani nawaachieni; amani yangu nawapa; niwapavyo mimi sivyo kama ulimwengu utoavyo. Msifadhaike mioyoni mwenu, wala msiwe na woga. Mlisikia ya kwamba mimi naliwaambia, Naenda zangu, tena naja kwenu. Kama mngalinipenda, mngalifurahi kwa sababu naenda kwa Baba; kwa maana Baba ni mkuu kuliko mimi. Na sasa nimewaambia kabla halijatokea, kusudi litakapotokea mpate kuamini. Mimi sitasema nanyi maneno mengi tena, kwa maana yuaja mkuu wa ulimwengu huu, wala hana kitu kwangu. Lakini ulimwengu ujue ya kuwa nampenda Baba; na kama vile Baba alivyoniamuru; ndivyo nifanyavyo. Ondokeni, twendeni zetu.

Maoni


Ingia utoe maoni