Masomo ya Misa
Jumatatu ya Oktava ya Pasaka (Jumatatu, Aprili 10, 2023)
Mdo 2:14, 22–32
Petro alisimama pamoja na wale kumi na mmoja, akapaza sauti yake, akawaambia, Enyi watu wa Uyahudi, na ninyi nyote mkaao Yerusalemu, lijueni jambo hili, mkalisikilize maneno yangu. Enyi waume wa Israeli, sikilizeni maneno haya; Yesu wa Nazareti, mtu aliyedhihirishwa kwenu na Mungu kwa miujiza na ajabu na ishara, ambazo Mungu alizifanya kwa mkono wake kati yenu, kama ninyi wenyewe mnavyojua; mtu huyu alipotolewa kwa shauri la Mungu lililokusudiwa, na kwa kujua kwake tangu zamani, ninyi mkamsulibisha kwa mikono ya watu wabaya, mkamwua; ambaye Mungu alimfufua, akaufungua uchungu wa mauti, kwa sababu haikuwezekana ashikwe nao. Maana Daudi ataja habari zake. Nalimwona Bwana mbele yangu sikuzote, kwa kuwa yuko upande wa mkono wangu wa kuume, nisitikisike. Kwa hiyo moyo wangu ukapendezewa, ulimi wangu ukafurahi; tena mwili wangu nao utakaa katika matumaini. Kwa maana hutaiacha roho yangu katika kuzimu; wala hutamtoa Mtakatifu wako aone uharibifu. Umenijulisha njia za uzima; utanijaza furaha kwa uso wako. Waume, ndugu zangu, mniwie radhi, niseme kwa ujasiri mbele yenu habari za baba yetu mkuu, Daudi, ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa alifariki akazikwa, na kaburi lake liko kwetu hata leo. Basi kwa kuwa ni nabii, akijua ya kuwa Mungu amemwapia kwa kiapo, ya kwamba katika uzao wa viuno vyake akamketisha mmoja katika kiti chake cha enzi; yeye mwenyewe akitangulia kuyaona haya, alitaja habari za kufufuka kwake Kristo, ya kwamba roho yake haikuachwa kuzimu, wala mwili wake haukuona uharibifu. Yesu huyo Mungu alimfufua, na sisi sote tu mashahidi wake.
Zab 16:1–2, 5, 7–11
Mungu unihifadhi mimi,
Kwa maana nakukimbilia Wewe.
Nimemwambia Bwana, Ndiwe Bwana wangu;
Bwana ndiye fungu la posho langu, na la kikombe changu;
Wewe unaishika kura yangu.
(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia wewe.
Nitamhimidi Bwana aliyenipa shauri,
Naam, mtima wangu umenifundisha usiku.
Nimemweka Bwana mbele yangu daima,
Kwa kuwa yako kuumeni kwangu, sitaondoshwa.
(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia wewe.
Kwa hiyo moyo wangu unafurahi,
Nao utukufu wangu unashangilia,
Naam, mwili wangu nao utakaa kwa kutumaini.
Maana hutaiachaia kuzimu nafsi yangu.
Wala hutamtoa mtakatifu wako aone uharibifu.
(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia wewe.
Utanijulisha njia ya uzima;
Mbele za uso wako ziko furaha tele;
Na katika mkono wako wa kuume mna mema ya milele.
(K) Mungu unihifadhi mimi, kwa maana nakukimbilia wewe.
Zab 118:24
Aleluya, aleluya,
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana, tutaishangilia na kuifurahia.
Aleluya.
Mt 28:8–15
Wanawake waliondoka upesi kutoka kaburini, kwa hofu na furaha nyingi, wakaenda mbio kuwapasha wanafunzi wake habari. Na tazama, Yesu akakutana nao, akisema, Salamu! Wakakaribia wakamshika miguu, wakamsujudia. Kisha Yesu akawaambia, Msiogope; enendeni, mkawaambie ndugu zangu waende Galilaya, ndiko watakakoniona. Nao wale walipokuwa wakienda, tazama, baadhi ya askari waliingia mjini, wakawapasha wakuu wa makuhani habari za mambo yote yaliyotendeka. Wakakusanyika pamoja na wazee, wakafanya shauri, wakawapa askari fedha nyingi, wakisema, Semeni, ya kwamba wanafunzi wake walikuja usiku, wakamwiba, sisi tulipokuwa tumelala. Na neno hili likisikilikana kwa liwali, sisi tutasema naye, nanyi tutawaondolea wasiwasi. Basi wakazitwaa zile fedha, wakafanya kama walivyofundishwa. Na neno hilo likaenea kati ya Wayahudi hata leo.
Maoni
Ingia utoe maoni