Masomo ya Misa
KUMBUKUMBU YA MT. FRANSISKO WA ASSISI (Jumanne, Oktoba 04, 2016)
Gal. 1:13 – 24
Mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu. Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu. Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake, alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu; wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski. Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano. Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana. Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo. Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia. Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri Imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.
Zab. 139:1 – 3, 13 – 14
Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
Wewe wajua kuketi kwangu na kuondoka kwangu;
Umelifahamu zazo langu tokea mbali.
Umepepeta kwenda kwangu na kulala kwangu,
Umeelewa na njia zangu zote.
(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.
Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.
Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika.
(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.
Maana Wewe ndiwe uliyeniumba mtima wangu,
Uliniunga tumboni mwa mama yangu.
Nitakushukuru kwa kuwa nimeumbwa
Kwa jinsi ya ajabu ya kutisha.
(K) Uniongoze, Ee Bwana, katika njia ya milele.
Yn. 14:5
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema:
mimi ndimi njia,
na ukweli, na uzima;
mtu haji kwa Baba,
ila kwa njia ya mimi.
Aleluya.
Lk. 10:38-42
Yesu aliingia katika kijiji kimoja; mwanamke mmoja jina lake Martha akamkaribisha nyumbani kwake. Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake. Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi; akamwendea, akasema, Bwana, huoni vibaya hivyo ndugu yangu alivyoniacha nitumike peke yangu? Basi mwambie anisaidie. Bwana akajibu akamwambia, Martha, Martha, unasumbuka na kufadhaika kwa ajili ya vitu vingi; lakini kinatakiwa kitu kimoja tu; na Mariamu amelichagua fungu lililo jema, ambalo hataondolewa.
Maoni
Ingia utoe maoni