Ijumaa. 22 Novemba. 2024

Tafakari

Jumanne, Oktoba 04, 2016

Jumanne, Oktoba 4, 2016.
Juma la 27 la Mwaka


Kumbukumbu ya Mt. Fransisko wa Assisi

Gal 1:13-24;
Zab 139: 1-3, 13-15;
Lk 10: 38-42.


KUMWELEKEA YESU!

Wakati Yesu alivyo watembelea Martha na Maria, Martha alikuwa akijishughulisha jikoni na pale Maria anakaa karibu na miguu ya Yesu huku akimsikiliza akiongea. Martha anamuomba Yesu amwambie Maria amsaidie. Yesu anamwambia Martha ana hofu na mambo mengi, wakati Maria amechagua njia sahihi zaidi. Tunaweza kushangaa kwani Martha hakuwa anafanya jambo lilo sahihi ambalo angepaswa kufanya?

Katika maisha yetu ya kila siku pia, mara nyingi tunafanya kazi tena na tena na wakati mwingine tunasahau kwanini kumekuwa na muda maalumu wa kazi. Watu wa ndoa wake kwa waume, wanapoteza muda mwingi katika kazi, na kuwa na muda kidogo tena sana wakuwa pamoja wao kwa wao na pia kuwa na watoto wao. Mapadre na wale wa maisha ya wakfu, hujikuta wanakuwa na muda mwingi wa kufanya utume na kazi nyingi na hata kuwa na muda mchache wakuwa pamoja na kwasababu ya kuchoka huenda kuacha kusali. Na hii huaribu maisha ya jumuiya kwasababu muda wa kupanga mambo pamoja hukosekana. Leo tujiunge na Mt. Fransisko alivyo waambia ndugu zake, “roho ya kazi isizime roho ya sala”. Siku zote waweza kujikuta muda hautoshi wa kumaliza kazi, hivyo ni bora kuwa na kiasi kwa kila kitu bila kusahau lilo la muhimu zaidi ambalo tutaliishi baada ya maisha yetu hapa duniani.
Mt. Fransisko wa Assisi tunaye mwadhimisha leo ni mtakatifu ambaye amegusa sana maisha ya wengi hasa baada ya wongofu wake. Ni mtakatifu ambaye anaheshimiwa sana na watu wengi mno katika Kanisa, na mashirika yalio chini yake ni mengi sana. Hii ni kwasababu, Neema ya Mungu ilivyo mtembelea alishirikiana nayo na hata kufikia hali ya juu kabisa ya maisha ya kiroho ambayo yanaendana na fadhila za Injili Takatifu, usafi wa moyo, unyenyekevu, kujikatalia na kutoshikamana na mambo ya dunia. Mt. Fransisko alimuisihi Kristo mpaka akafanana na Kristo mwenyewe, na hata siku za mwisho za maisha yake akiwa anasali katika mlima Laverna Yesu alimzawadia madonda matakatifu katika mwili wake. Mtakatifu Fransisko aliwapenda maskini kiasi cha kutoa hata mali ya Baba yake na kuwagawia. Katika jamii zetu siku hizi tunadhani kushirikiana na maskini ni kujidhalilisha, tunataka tu tukae na wale wenye mali wale ambao tukiwapa wana uwezo wakuturudishia baadae. Hali hii imekuwa katika akili za vijana na wanaona hayo ndio maisha.

Mtakatifu huyu ni mfano mzuri sana kwa vijana wa kike na wakiume wanaodhani maisha ya kushikamana na mitindo mbali mbali inayotoka kila kukicha ndio hali ya juu ya maisha. Yapo maovu mengi yanayo onekana wazi kwa vijana katika nyakati zetu, mfano mambo ya ujambazi na kutumia silaha mfano tumesikia kuhusu –Mungiki Nairobi Kenya, Panya Roads na Vibaka Dar es salam, Mbio za Vijiti Musoma, Nyoka boys na Dogos Mererani na hata Boko-Haramu Nigeria haya yote yanatendwa na vijana. Hii ni kwasababu wanakosa zile tunu na fadhila za Injili ndani mwao, wanatamani maisha ya juu au utajiri wa haraka kwasababu duniani na malezi tuliowapa yameshawafundisha kwamba kuwa na magari mengi, kubadili nguo za kila aina na fasheni mbali mbali na mengine mengi ndio mtindo wa maisha, hii inawafanya waanze kutafuta mali kwa njia yeyote ile bila kujali ni sahihi au la. Kwa maisha ya Mtakatifu Fransiko yawe mfano kwetu wote na vijana wote, maisha ya unyenyekevu, maisha ya usafi wa moyo, maisha ya kujikatalia nakutokushikamana na malimwengu. Tukiyashika haya kila mwadamu atakuwa akitafuta uzuri wa mwenzake. Ubinafsi na kujilimbikizia havitakuwepo na uhalifu au maovu yataondoka kabisa. Mt. Fransiko pia alivipenda viumbe sisi nasi tupende viumbe na tulinde mazingira yetu.

Katika Injili Maria anachukua nafasi sahihi kwa kuchagua kubaki na Yesu. Na hapa tunaona matokeo ya uchaguzi wa mtu binafsi. Uchaguzi wa mtu unampa uzima wa milele au kifo na uharibifu. Kila mmoja wetu anaitwa kufanya uchaguzi sahihi kwa maisha yake. Mfanye Mungu rafiki yako na utafurahia urafiki wake milele.

SALA: Ee Bwana nichague wewe uliye njia sahihi. Amina

Maoni


Ingia utoe maoni