Masomo ya Misa
Jumanne ya 1 ya Mwaka (Jumanne, Januari 10, 2023)
Ebr 2:5–12
Mungu hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali Fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, umemvika taji ya utukufu na heshima, umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; umeweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake, ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.
Zab 8:2, 5–9
Wewe, Mungu, Bwana wetu,
Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
Mtu ni kitu gani hata umkumbuke,
Na binadamu hata umwangalie?
(K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi ya mikono yako.
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako.
(K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi ya mikono yako.
Umevitia vitu vyote chiini ya miguu yake,
Kondoo, na ng’ombe wote pia,
Naam, na wanyama wa kondeni,
Ndege wa angani, na samaki wa baharini,
Na kila kipitiacho njia za baharini.
(K) Umemtawaza Mwanao juu ya kazi ya mikono yako.
Ebr 4:12
Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.
Mk 1:21-28
Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akifundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.
Maoni
Ingia utoe maoni