Masomo ya Misa
Jumamosi baada ya Epifania (Jumamosi, Januari 07, 2023)
1Yn 5:14-21
Wapenzi: Huu ndio ujasiri tulio nao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawasawa na mapenzi yake, atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Mtu akimwona ndugu yake anatenda dhambi isiyo ya mauti, ataomba, na Mungu atampa uzima kwa ajili ya hao watendao dhambi isiyo ya mauti. Iko dhambi iliyo ya mauti. Sisemi ya kwamba ataomba kwa ajili ya hiyo. Kila lisilo la haki ni dhambi, na dhambi iko isiyo ya mauti. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi; bali yeye aliyezaliwa na Mungu hujilinda, wala yule mwovu hamgusi. Twajua ya kuwa sisi tu wa Mungu; na dunia yote pia hukaa katika yule mwovu. Nasi twajua kwamba Mwana wa Mungu amekwisha kuja, naye ametupa akili kwamba tumjue yeye aliye wa kweli, nasi tumo ndani yake yeye aliye wa kweli, yaani, ndani ya Mwana wake Yesu Kristo. Huyu ndiye Mungu wa kweli, na uzima wa milele. Watoto wadogo, jilindeni nafsi zenu na sanamu.
Zab 149:1-6, 9
Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Sifa zake katika kusanyiko la watauwa.
Israeli na amfurahie Yeye aliyemfanya,
Wana wa Sayuni na wamshangilie mfalme wao.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Na walisifu jina lake kwa kucheza,
Kwa matari na kinubi wamwimbie.
Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake,
Huwapamba wenye upole kwa wokovu.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Watauwa na waushangilie utukufu,
Waimbe kwa sauti kuu vitandani mwao.
Sifa kuu za Mungu na ziwe vinywani mwao,
Na upanga mkali kuwili mikononi mwao.
Kuwafanyia hukumu iliyoandikwa;
Hiyo ndiyo heshima ya watauwa wake wote.
(K) Kwa kuwa Bwana awaridhia watu wake
Lk 7:16
Aleluya, aleluya
Nabii mkuu ametokea kwetu; Na Mungu amewaangalia watu wote
Aleluya
Yn 2:1-11
Wakati ule, palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo. Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake. Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai. Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia. Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni. Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu. Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu. Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka. Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi, akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa. Mwanzo huo wa ishara Yesu aliufanya huko Kana ya Galilaya, akaudhihirisha utukufu wake, nao wanafunzi wake wakamwamini.
Maoni
Ingia utoe maoni