Masomo ya Misa
Sikukuu ya Familia Takatifu (Ijumaa, Desemba 30, 2022)
Ybs 3:2-6, 12-14
Bwana amempa baba utukufu mintarafu wana , na kuithibitisha haki ya mama mintarafu watoto. Anayemheshimu baba yake atafanya malipizi ya dhambi, naye anayemtukuza mama yake, huweka akiba iliyo azizi. Anayemheshimu babaye atawafurahia watoto wake mwenyewe, na siku ya kuomba dua atasikiwa. Anayemtukuza baba yake ataongezewa siku zake; akimsikiliza Bwana, atamstarehesha mamaye.Mwanangu , umsaidie baba yako katika uzee wake ; wala usipate kumhuzunisha siku zote za maisha yake.Akiwa amepungukiwa na ufahamu umwie kwa upole, wala usimdharau iwapo wewe u mzima sana; kwa maana sadaka apewayo baba haitasahaulika, na badala ya dhambi itahesabiwa kwa kukudhibitisha.
Zab 128:1-5
Heri kila mtu amchaye BWANA,
Aendaye katika njia yake.
Taabu ya mikono yako hakika utaila;
Utakuwa heri, na kwako kwema.
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye katika njia zake
Mkeo atakuwa kama mzabibu uzaao,
Vyumbani mwa nyumba yako.
Wanao kama miche ya mizeituni
Wakiizunguka meza yako.
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye katika njia zake
Tazama, atabarikiwa hivyo,
yule amchaye BWANA.
BWANA akubariki toka Sayuni;
Uone uheri wa Yerusalemu
siku zote za maisha yako;
(K) Heri kila mtu amchaye BWANA, aendaye katika njia zake.
Kol 3:12-21
Ndugu zangu, kwa kuwa mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu wapendwao, jivikeni moyo wa rehema, utu wema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, mkichukuliana, na kusameheana, mtu akiwa na sababu ya kumlaumu mwenzake; kama Bwana alivyowasamehe ninyi, vivyo na ninyi. Zaidi ya hayo yote jivikeni upendo, ndio kifungo cha ukamilifu. Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu; ndiyo mliyoitiwa katika mwili mmoja; tena iweni watu wa shukrani. Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni; huku mkimwimbia Mungu kwa neema mioyoni mwenu. Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye. Ninyi wake, watiini waume zenu, kama ipendezavyo katika Bwana. Ninyi waume, wapendeni wake zenu msiwe na uchungu nao. Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote; maana jambo hili lapendeza katika Bwana. Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.
Kol 3:15, 16
Aleluya ,aleluya
Na amani ya Kristo iamue mioyoni mwenu;
Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu
Aleluya
Lk 2:41-52
Wazee wake Yesu huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka. Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu; na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari. Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao; na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, ameketi katikati ya waalimu, akiwasikiliza na kuwauliza maswali. Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni. Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake. Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Maoni
Ingia utoe maoni