Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumamosi ya 22 ya Mwaka (Jumamosi, Septemba 03, 2022)  

Somo la 1

1Kor 4:6-15

Ndugu zangu, mambo hayo nimeyafanya kuwa mfano wa mimi na Apolo kwa ajili yenu, ili kwamba kwa mfano wetu mpate kujifunza kutokupita yale yaliyoandikwa; ili mmoja wenu asijivune kwa ajili ya huyu, kinyume cha mwenziwe. Maana ni nani anayekupambanua na mwingine? Nawe una nini usichokipokea? Lakini iwapo ulipokea, wajisifia nini kana kwamba hukupokea? Mmekwisha kushiba, mmekwisha kupata utajiri, mmemiliki pasipo sisi. Naam, laiti mngemiliki, ili sisi nasi tumiliki pamoja nanyi! Maana nadhani ya kuwa Mungu ametutoa sisi mitume mwisho, kama watu waliohukumiwa wauawe; kwa sababu tumekuwa tamasha kwa dunia; kwa malaika na wanadamu. Sisi tu wapumbavu kwa ajili ya Kristo, lakini ninyi ni wenye akili katika Kristo; sisi tu dhaifu, lakini ninyi mna nguvu; ninyi mna utukufu, lakini sisi hatupati heshima. Hata saa hii ya sasa, tuna njaa na kiu, tu uchi, twapigwa ngumi, tena hatuna makao; kisha twataabika tukifanya kazi kwa mikono yetu wenyewe. Tukitukanwa twabariki, tukiudhiwa twastahimili; tukisingiziwa twasihi; tumefanywa kama takataka za dunia, na tama ya vitu vyote hata sasa. Siyaandiki hayo ili kuwatahayarisha; bali kuwaonya kama watoto niwapendao. Kwa kuwa ijapokuwa mna waalimu kumi elfu katika Kristo, walakini hamna baba wengi. Maana mimi ndimi niliyewazaa katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili.

Wimbo wa Katikati

Zab 145:17-21

Bwana ni mwenye haki katika njia zake zote,
Na mwenye fadhili juu ya kazi zake zote.
Bwana yu karibu na wote wamwitao,
Wote wamwitao kwa uaminifu.
(K) Bwana yu karibu na wote wamwitao.

Atawafanyia wamchao matakwa yao,
Naye atakisikia kilio chao na kuwaokoa.
Bwana huwahifadhi wote wampendao,
Na wote wasio haki atawaangamiza.
(K) Bwana yu karibu na wote wamwitao.

Kinywa changu kitazinena sifa za Bwana;
Wote wenye mwili na walihimidi jina lake takatifu milele na milele.
(K) Bwana yu karibu na wote wamwitao.

Shangilio

Yn 14:6

Aleluya, Aleluya
Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya

Injili

Lk 6:1-5

Ilikuwa siku ya sabato moja alikuwa akipita katika mashamba, wanafunzi wake wakawa wakivunja masuke na kuyala, wakiyapukusa-pukusa mikononi mwao. Basi baadhi ya Mafarisayo wakawaambia, Mbona mnafanya lisilo halali siku ya sabato? Yesu akawajibu akawaambia, Hamkulisoma hata hilo alilolifanya Daudi, alipokuwa na njaa, yeye na wale aliokuwa nao? Jinsi alivyoingia katika nyumba ya Mungu, akaitwaa mikate ile ya Wonyesho, akaila akawapa na hao wenziwe, ambayo si halali kuila ila kwa makuhani peke yao. Akawaambia, Mwana wa Adamu ndiye Bwana wa sabato.

Maoni


Ingia utoe maoni