Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 22 ya Mwaka (Jumapili, Agosti 28, 2022)  

Somo la 1

Ybs 3:17-20, 28-29

Mwanangu, wakati wa kufanikiwa uendelee katika unyenyekevu; hivyo utapendwa kuliko mwenye ukarimu. Kadiri ulivyo mkuu uzidi kujinyenyekesha, nawe utapata kibali machoni pa Bwana; kwa maana rehema zake Bwana zi kuu, na siri yake ni kwa wanyenyekevu. Msiba wa mwenye kiburi hauleti kupona, Mche wa uovu umepandika ndani yake. Moyo wa busara utatambua mithali, Na sikio sikivu ni tamaa ya mtaalamu.

Wimbo wa Katikati

Zab 68:3-6, 9-10

Wenye haki watafurahi,
Na kuushangilia uso wa Mungu,
Naam, hupiga kelele kwa furaha.
Mwimbieni Mungu, lisifuni jina lake,
Furahini katika Bwana, shangilieni mbele zake.
(K) Ee Mungu, Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa

Baba wa yatima na mwamuzi wa wajane,
Mungu katika kao lake takatifu.
Mungu huwakalisha wapweke nyumbani;
Huwatoa wafungwa wakae hali ya kufanikiwa;
(K) Ee Mungu, Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa

Ee Mungu, ulinyesha mvua ya neema;
Urithi wako ulipochoka uliutia nguvu.
Kabila yako ilifanya kao lake huko;
Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa.
(K) Ee Mungu, Kwa wema wako uliwahifadhi walioonewa

Somo la 2

Ebr 12:18-19, 22-24

Hamkufikilia mlima uwezao kuguswa, uliowaka moto, wala wingu jeusi, na giza, na tufani, na mlio wa baragumu na sauti ya maneno; ambayo wale walioisikia walisihi wasiambiwe neno lo lote lingine; Bali ninyi mmeufikilia mlima Sayuni, na mji wa Mungu aliye hai, Yerusalemu wa mbinguni, na majeshi ya malaika elfu nyingi, mkutano mkuu na kanisa la wazaliwa wa kwanza walioandikwa mbinguni, na Mungu mwamuzi wa watu wote, na roho za watu wenye haki waliokamilika, na Yesu mjumbe wa agano jipya, na damu ya kunyunyizwa, inenayo mema kuliko ile ya Habili.

Shangilio

Mt 11:25

Aleluya, aleluya
Ninakushukuru Baba, Bwana wa mbingu na nchi, Kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili, Ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya

Injili

Lk 14:1, 7-14

Yesu alipoingia ndani ya nyumba ya mtu mmoja miongoni mwa wakuu wa Mafarisayo siku ya sabato, ale chakula, walikuwa wakimvizia. Akawaambia mfano wale walioalikwa, alipoona jinsi walivyochagua viti vya mbele; akisema, Ukialikwa na mtu arusini, usiketi katika kiti cha mbele; isiwe kwamba amealikwa mtu mwenye kustahiwa kuliko wewe, akaja yule aliyewaalika wewe na yeye, na kukuambia, Mpishe huyu! Ndipo utakapoanza kwa haya kushika mahali pa nyuma. Bali ukialikwa, nenda ukaketi mahali pa nyuma, ili ajapo yule aliyekualika akuambie, Rafiki yangu, njoo huku mbele zaidi; ndipo utakapokuwa na utukufu mbele ya wote walioketi pamoja nawe. Kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa. Akamwambia na yule aliyemwalika, Ufanyapo chakula cha mchana au cha jioni, usiwaite rafiki zako, wala ndugu zako, wala jamaa zako, wala jirani zako wenye mali; wao wasije wakakualika wewe ukapata malipo. Bali ufanyapo karamu waite maskini, vilema, viwete, vipofu, nawe utakuwa heri, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa; kwa maana utalipwa katika ufufuo wa wenye haki.

Maoni


Ingia utoe maoni