Alhamisi. 25 Aprili. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 19 ya Mwaka (Jumanne, Agosti 09, 2022)  

Somo la 1

Eze 2:8–3:4

Ezekieli aliisikia sauti, ikamwambia: Mwanadamu, sikia neno hili ninalokuambia; usiwe wewe mwenye kuasi kama nyumba ile yenye kuasi; funua kinywa chako, ule nikupacho. Nami nilipotazama, mkono ulinyoshwa kunielekea; na tazama, gombo la chuo lilikuwa ndani yake. Akalikunjua mbele yangu; nalo lilikuwa limeandikwa ndani na nje; ndani yake yalikuwa yameandikwa maombolezo, na vilio, na ole! Akaniambia, Mwanadamu, kula uonacho; kula gombo hili, kisha enenda ukaseme na wana wa Israeli. Basi nikafunua kinywa changu, naye akanilisha lile gombo. Akaniambia, Mwanadamu, lisha tumbo lako, ulijaze tumbo lako kwa hili gombo nikupalo. Ndipo nikalila, nalo kinywani mwangu lilikuwa tamu, kama utamu wa asali. Akaniambia, Mwanadamu, haya! Waendee wana wa Israeli, ukawaambie maneno yangu.

Wimbo wa Katikati

Zab 119:14, 24, 72, 103, 111, 131

Nimeifurahia njia ya shuhuda zako,
Kana kwamba ni mali mengi.
Shuhuda zako nazo ndizo furaha yangu,
Na washauri wangu.
(K) Mausi yako ni matamu sana kwangu.

Sheria ya kinywa chako ni njema kwangu,
Kuliko maelfu ya dhahabu na fedha.
Mausia yako ni matamu sana kwangu,
Kupita asali kinywani mwangu.
(K) Mausi yako ni matamu sana kwangu.

Shuhuda zako nimezifanya urithi wa milele,
Maana ndizo changamko la moyo wangu.
Nalifunua kinywa changu nikakweta,
Maana naliyatamani maagizo yako.
(K) Mausi yako ni matamu sana kwangu.

Shangilio

Yn 17:17

Aleluya, aleluya,
Neno lako ndiyo kweli, Ee Bwana, ututakase kwa ile kweli.
Aleluya.

Injili

Mt 18:1–5, 10 , 12, 14

Wanafunzi walimwendea Yesu wakisema, Ni nani basi aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni? Akaita mtoto mmoja, akamweka katikati yao, akasema, Amin, nawaambia, Msipoongoka na kuwa kama vitoto, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Basi, yeyote ajinyenyekeshaye mwenyewe kama mtoto huyu, huyo ndiye aliye mkuu katika ufalme wa mbinguni. Na yeyote atakayempokea mtoto mmoja mfano wa huyu kwa jina langu, anipokea mimi. Angalieni msidharau mmojawapo wadogo hawa; kwa maana nawaambia ya kwamba malaika zao mbinguni sikuzote huutazama uso wa Baba yangu aliye mbinguni. Mwaonaje? Mtu akiwa na kondoo mia, mmoja akampotea, je! Hawaachi wale tisa na tisini, akaenda milimani, na kumtafuta yule aliyepotea? Vivyo hivyo haipendezwi mbele za Baba yenu aliye mbinguni kwamba mmoja wa wadogo hawa apotee.

Maoni


Ingia utoe maoni