Masomo ya Misa
Dominika ya 15 ya Mwaka (Jumapili, Julai 10, 2022)
Kumb 30:10–14
Ukiwa utaifuata sauti ya Bwana, Mungu wako, kwa kuyashika maagizo yake, na amri zake zilizoandikwa katika chuo hiki cha torati; ukimwelekea Bwana, Mungu wako, kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote. Kwa maana maagizo haya nikuagizayo leo, si mazito mno kwako, wala si mbali. Si mbinguni, hata useme, Ni nani atakayetupandia mbinguni akatuletee, aje atuambie tusikie, tupate kuyafanya? Wala si ng’ambo ya pili ya bahari, hata useme. Ni nani atakayetuvukia bahari, akatuletee, aje atuambie, tusikie, tupate kuyafanya? Lakini neno li karibu nawe sana, li katika kinywa chako na moyo wako, upate kulifanya.
Zab 68:13, 16, 29–30, 32–33, 35–36
Nami maombi yangu nakuomba Wewe Bwana,
Wakati ukupendezao; Ee Mungu.
Kwa wingi wa fadhili zako unijibu.
Katika kweli ya wokovu wako.
Ee Bwana, unijibu, maana fadhili zako ni njema,
Kwa kadiri ya rehema zako unielekee.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Nami niliye maskini na mtu wa huzuni.
Mungu, wokovu wako utaniinua.
Nitalisifu jina la Mungu kwa wimbo,
Nami nitamtukuza kwa shukrani.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Walioonewa watakapoona watafurahi;
Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kwa kuwa Bwana huwasikia wahitaji.
Wala hawadharau wafunga wake.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Maana Mungu ataiokoa Sayuni, na kuijenga miji ya Yuda,
Wazao wa watumishi wake watairithi,
Nao walipendao jina lake watakaa humo.
(K) Enyi mmtafutao Mungu, mioyo yenu ihuishwe.
Kol 1:15–20
Kristo ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni viti vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye. Naye ndiye kichwa cha mwili, yaani, cha kanisa; naye ni mwanzo, ni mzaliwa wa kwanza katika wafu, ili kwamba awe mtangulizi katika yote. Kwa kuwa katika yeye ilipendeza utimilifu wote ukae; na kwa yeye kuvipatanisha vitu vyote na nafsi yake, akiisha kufanya Amani kwa damu ya msalaba wake; kwa yeye, ikiwa ni vitu vilivyo juu ya nchi, au vilivyo mbinguni.
Mdo 16:14
Aleluya, aleluya!
Fungua moyo wetu, Ee Bwana, ili tuyatunze maneno ya Mwanao.
Aleluya.
Lk 10:25–37
Siku ile, mwanasheria mmoja alisimama amjaribu, akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele? Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje? Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako. Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani? Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyanyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa. Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipitia kando. Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapitia kando. Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia, akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza. Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na chochote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa. Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake, yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi? Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo.
Maoni
Ingia utoe maoni