Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 14 ya Mwaka (Ijumaa, Julai 08, 2022)  

Somo la 1

Hos 14:2–9

Bwana anasema: Chukueni maneno pamoja nanyi, mkamrudie Bwana; mkamwambie, Ondoa maovu yote, uyatakabali yaliyo mema; na hivyo ndivyo mtakavyotoa sadaka za midomo yetu kana kwamba ni ng'ombe. Ashuru hatatuokoa; hatutapanda farasi; wala hatutaiambia tena kazi ya mikono yetu, Ninyi ndinyi miungu yetu; maana kwako wewe wasio na baba hupata rehema. Mimi nitawaponya kurudi nyuma kwao; nitawapenda kwa ukunjufu wa moyo; kwa maana hasira yangu imemwacha. Nitakuwa kama umande kwa Israeli; naye atachanua maua kama nyinyoro, na kuieneza mizizi yake kama Lebanoni. Matawi yake yatatandaa, na uzuri wake utakuwa kama uzuri wa mzeituni, na harufu yake kama Lebanoni. Na wao wakaao chini ya uvuli wake watarejea; watafufuka kama ngano, na kuchanua maua kama mzabibu; harufu yake itakuwa kama harufu ya divai ya Lebanoni. Efraimu atasema, Mimi nina nini tena na sanamu? Mimi nimeitika, nami nitamwangalia. Mimi ni kama mberoshi wenye majani mabichi. Kwangu mimi yamepatikana matunda yako. Ni nani aliye na hekima, naye atayafahamu mambo haya? Ni nani aliye na busara, naye atayajua? Kwa maana njia za Bwana zimenyoka, nao wenye haki watakwenda katika njia hizo; bali waasio wataanguka ndani yake.

Wimbo wa Katikati

Zab 51:1–2,6–7,10–11,15

Ee Mungu, unirehemu,
Sawasawa na fadhili zako.
Kiasi cha wingi wa rehema zako,
Uyafute makosa yangu.
Unioshe kabisa na uovu wangu,
Unitakase dhambi zangu.
(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

Tazama, wapendezwa na kweli iliyo moyoni,
Nawe utanijulisha hekima kwa siri,
Unisafishe kwa hisopo nami nitakuwa safi,
Unioshe, nami nitakuwa mweupe kuliko theluji.
(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

Ee Mungu, uniumbie moyo safi,
Uifanye upya roho iliyotulia ndani yangu.
Usinitenge na uso wako,
Wala roho yako mtakatifu usiniondolee.
(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

Ee Bwana, uifumbue midomo yangu,
Na kinywa change kitazinena sifa zako.
(K) Ulimi wangu utaiimba haki yako.

Shangilio

1Pet 1:25

Aleluya, aleluya,
Neno la Bwana hudumu hata milele, na neno hilo ni neno lile jema lililohubiriwa kwenu.
Aleluya.

Injili

Mt 10:16–23

Yesu aliwaambia mitume wake: Angalieni, mimi nawatuma kama kondoo kati ya mbwa mwitu; basi iweni na busara kama nyoka, na kuwa watu wapole kama hua. Jihadharini na wanadamu; kwa maana watawapeleka mabarazani, na katika masinagogi yao watawapiga; nanyi mtachukuliwa mbele ya maliwali na wafalme kwa ajili yangu, kuwa ushuhuda kwao na kwa mataifa. Lakini hapo watakapowapeleka, msifikirifikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema. Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu ndani yenu. Na ndugu atamsaliti nduguye ili auawe, na baba atamsaliti mwana, na wana watawainukia wazazi wao, na kuwafisha. Nanyi mtakuwa mkichukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu; lakini mwenye kuvumilia hata mwisho, ndiye atakayeokoka. Lakini watakapowafukuza katika mji huu, kimbilieni mwingine; kwa maana ni kweli nawaambia, Hamtaimaliza miji ya Israeli, hata ajapo Mwana wa Adamu.

Maoni


Ingia utoe maoni