Jumatatu. 25 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Ijumaa ya 11 ya Mwaka (Ijumaa, Juni 17, 2022)  

Somo la 1

2 Fal. 11:1-4, 9-18, 20

Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme. Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia, akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia, akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa, yeye na mlezi wake, na kuwatia katika chumba cha kulala; wakamficha usoni pa Athalia, basi kwa hiyo hakuuawa. Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa Bwana, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi. Hata mwaka wa saba Yehoyada akatujma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme. Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani. Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa Bwana. Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote. Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, Mfalme na aishi. Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa Bwana; akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina! Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; nay yeyote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa Bwana. Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko. Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya Bwana na mfalme na watu, ili wawe watu wa Bwana; tena kati ya mfalme na watu. Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunjavunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka maakida juu ya nyumba ya Bwana. Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme.

Wimbo wa Katikati

Zab. 132: 11 – 14, 17 – 18

Bwana amemwapia Daudi neno la kweli,
Hatarudi nyuma akalihalifu,
Baadhi ya wazao wa mwili wako
Nitawaweka katika kiti chako cha enzi.
(K) Bwana ameichagua Sayuni, ameitamani akae ndani yake.

Wanao wakiyashika maagano yangu,
Na shuhuda nitakazowafundisha;
Watoto wao nao wataketi
Katika kiti chako cha enzi milele.
(K) Bwana ameichagua Sayuni, ameitamani akae ndani yake.

Kwa kuwa Bwana ameichagua Sayuni,
Ameitamani akae ndani yake.
Hapo ndipo mahali pangu pa raha milele,
Hapo nitakaa kwa maana nimepatamani.
(K) Bwana ameichagua Sayuni, ameitamani akae ndani yake.

Hapo nitamchipushia Daudi pembe,
Na taa nimemtengenezea masihi wangu.
Adui zake nitawavika aibu,
Bali juu yake taji yake itasitawi.
(K) Bwana ameichagua Sayuni, ameitamani akae ndani yake.

Shangilio

Zab. 119: 18

Aleluya, aleluya,
Unifumbue macho yangu niyatazame maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya.

Injili

Mt. 6:19 – 23

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako. Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru. Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo!

Maoni


Ingia utoe maoni