Jumapili. 24 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Dominika ya 23 ya Mwaka (Jumapili, Septemba 04, 2016)  

Somo la 1

1 Hek 9:13-19

Ni mtu yupi awezaye kulijua shauri la Mungu? Au ni nani atakayeelewa na mapenzi yake? Kwa kuwa mawazo ya wanadamu yana woga, na makusudi yetu yanaelekea kishindwa; na mwili wenye uharibifu huigandamiza roho, na kiwiliwili cha kidunia huzilemea akili zilizosongwa na masumbuko. Kwa shida tu twayapambanua yaliyoko duniani, na yaliyo karibu nasi ni kazi kuyaona; lakini yaliyoko mbinguni ni nani aliyegundua? Naye ni yupi aliyeyavumbua mashauri yako, isipokuwa ulimpa Hekima na kumplelekea Roho yako takatifu kutoka juu? Ndivyo miendo yao wakaao duniani iliyosafishwa, na wanadamu walivyofundishwa yakupendezavyo; hata na kwa Hekima wao wenyewe waliponyawa.

Wimbo wa Katikati

Zab 90:3-6, 12-14, 17

Wamrudisha mtu mavumbini, usemapo, Rudini, enyi wanadamu.
Maana miaka elfu machoni pako Ni kama siku ya jana ikiisha kupita,
Na kama kesha la usiku.
(K) Wewe, Bwana umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi

Wawagharikisha, huwa kama usingizi,
Asubuhi huwa kama majani yameayo.
Asubuhi yachipuka na kumea,
Jioni yakatika na kukauka.
(K) Wewe, Bwana umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi

Basi, utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima.
Ee Bwana urudi, hata lini? Uwahurumie watumishi wako.
(K) Wewe, Bwana umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi

Utushibishe asubuhi kwa fadhili zako,
Nasi tutashangilia na kufurahi siku zetu zote.
Na uzuri wa Bwana, Mungu wetu, uwe juu yetu,
Na kazi ya mikono yetu utufanyie thabiti,
Naam, kazi ya mikono yetu uithibitishe.
(K) Wewe, Bwana umekuwa makao yetu kizazi baada ya kizazi

Somo la 2

Flm 1: 9-10, 12-17

Paulo mzee, na sasa mfungwa wa Kristo Yesu pia. Nakusihi kwa ajili ya mtoto wangu niliyemzaa katika vifungo vyangu, yaani, Onesimo;niliyemtuma kwako, yeye mwenyewe, maana ni moyo wangu hasa; ambaye mimi nalitaka akae kwangu, apate kunitumikia badala yako katika vifungo vya Injili. Lakini sikutaka kutenda neno lo lote isipokuwa kwa shauri lako, ili kwamba wema wako usiwe kama kwa lazima, bali kwa hiari. Maana, labda ndiyo sababu alitengwa nawe kwa muda, ili uwe naye tena milele; tokea sasa, si kama mtumwa, bali zaidi ya mtumwa, ndugu mpendwa; kwangu mimi sana, na kwako wewe zaidi sana, katika mwili na katika Bwana. Basi kama ukiniona mimi kuwa mshirika nawe, mpokee huyu kama mimi mwenyewe.

Shangilio

Efe 1:17,18

Aleluya, aleluya
Ewe Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, uyatie nuru macho ya mioyo yetu,
Ili tujue tumaini la mwito wako jinsi lilivyo
Aleluya

Injili

Lk 14:25-33

Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki, wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhalika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

Maoni


Ingia utoe maoni